VIDEO: Mtandao maarufu China kuvitangaza vivutio vya Tanzania

Baadhi ya wafanyakazi wa mtandao wa Baidu wakicheza ngoma iliyokuwa ikipigwa na kikundi cha Nimujo muda mfupi baada ya kupokelewa nchini.

Muktasari:

  • Jitihada za kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania zashika kasi, picha za vivutio hivyo kuonyeshwa kwenye mtandao wa China

Dar es Salaam. Tanzania inakuwa nchi ya kwanza barani Afrika kupata nafasi ya vivutio vya utalii kuonekana kwenye  mtandao wa Baidu wa nchini China.

Hilo limedhihirika baada ya kampuni ya mtandao wa utafutaji ya Baidu ya China kuiweka Tanzania miongoni mwa nchi saba zitakazotangaziwa vivutio vyake vya utalii kwenye mtandao huo.

Mtandao huo ndiyo unaongoza kwa kutumiwa  China ukichukua zaidi ya asilimia 75 ya watumiaji wote wa intaneti nchini China.

Tayari timu ya wafanyakazi 12 wa mtandao huo wamewasili nchini Tanzania jana Alhamisi Agosti 22,2019 kwa ajili ya kupiga picha za maeneo ya vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania kwa ajili ya kuvionyesha kwa Wachina.

Timu hiyo itakuwa Tanzania kwa siku 11 ikizuru vivutio mbalimbali ikiwemo mbuga ya Serengeti, Bonde la Ngorongoro, makumbusho ya Bagamoyo na fukwe za Zanzibar.

Mkuu wa kitengo cha uhusiano Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Geofrey Tengeneza alisema mradi huo una maana kubwa kwa utalii wa Tanzania kwani utasaidia kuongeza idadi ya watalii kutoka China.

Alisema fursa hiyo itasaidia Tanzania kuliteka soko la utalii la China na kuwahamasisha watalii wengi kuja nchini baada ya kuviona vivutio vilivyopo kupitia picha.

“Tunaweza kusema hii ni fursa kubwa tuna kila sababu ya kushukuru kwa Tanzania kuwa sehemu ya mradi huu, urafiki wetu na China unazidi kuimarika hasa kwenye sekta hii ya utalii.” alisema

“Baidu ni mtandao mkubwa kule China yaani kama ilivyo Google sasa Wachina wanapotafuta kitu mtandaoni wanapitia Baidu, habari na picha kuhusu Tanzania kuwekwa humo ni hatua kubwa,” alisema

Alisema, “ Ina maana sasa wachina wataiona Tanzania kupitia picha na hilo litawashawishi kuja kutalii nchini kwetu, nia yetu ni kuliteka soko la utalii la China ambalo kwa sasa ndilo linaongoza kuwa na watalii wengi duniani.”

Tengeneza alisema China ni nchi inayoongoza kutoa watalii wengi duniani lakini ni idadi ndogo wanakuja kutalii Tanzania.

Mkalimani wa wafanyakazi hao ambaye pia ni raia wa China, Maria alisema ni fursa kubwa ambayo Tanzania imeipata kujitangaza kupitia mtandao huo.

“Uhusiano kati ya Tanzania na China unaendelea kukua, Tanzania ina madhari nzuri ya kuvutia, yakiwekwa kwenye Baidu Wachina wengi wataona na watatamani kuja,” alisema