Mtanzania anayedai anaweza kutibu virusi vya corona matatani

Friday February 14 2020

Mtanzania anayedai anaweza kutibu virusi vya corona matatani, Moses Mollel maarufu Nabii Namba Saba,virusi vya corona,maambukizi ya virusi vya corona,MwananchiHabari,vifo vya wagonjwa wa Corona,Corona,

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema itamchukulia hatua  Moses Mollel maarufu Nabii Namba Saba iwapo atashindwa kudhibitisha kauli yake  kuwa ana uwezo wa kutibu wenye maambukizi ya virusi vya corona.

Hayo yameelezwa na naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile katika ziara yake ya kikazi jijini Arusha.

Nabii Namba Saba, mkazi wa Ngaramtoni wilayani Arumeru mkoani Arusha amekuwa akijitangaza kuwa na dawa ya kutibu ugonjwa huo na kuweka mawasiliano yake  kwenye mitandao.

Dk Ndugulile amesema taarifa za mtu huyo zimesambaa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, kumtaka athibitishe.

Amesema Serikali imetuma wataalamu wake  kumsaka na kumhoji kama anavyo vibali vya kutoa huduma ya tiba na kujitangaza.

 “Kimsingi nimeiona hiyo taarifa ya huyo mtu  anayejiita Nabii Namba Saba kuwa ana dawa ya kutibu ugonjwa wa Corona, ila hapa Tanzania hatuna maambukizi yoyote ya ugonjwa huo tunachotaka huyo mtu  atuthibitishie uwezo wake wa kutibu huo ugonjwa wa corona,” amesema Dk Ndugulile.

Advertisement

Ameongeza kuwa iwapo atashindwa kuthibitisha atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Dk Ndugulile amesema  yeyote anayetoa tiba asili na mbadala lazima asajiliwe na Wizara ya Afya, dawa zake ziwe zimesajiliwa na Wizara hiyo na kusisitiza kuwa nabii huyo pia anapaswa kuthibitisha amesajiliwa wapi na lini.

 

 

Advertisement