Mtego anguko la Sumaye Chadema

 Frederick Sumaye

Muktasari:

Kuanguka kwa Frederick Sumaye katika uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti wa Kanda ya Pwani ya Chadema kunaweza kuwa na maelezo mepesi, “hiyo ndiyo demokrasia”.


Dar es Salaam. Kuanguka kwa Frederick Sumaye katika uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti wa Kanda ya Pwani ya Chadema kunaweza kuwa na maelezo mepesi, “hiyo ndiyo demokrasia”.

Lakini hayo hayatoshi kuelezea kuanguka kwa mtu ambaye alishika nafasi ya mtendaji mkuu wa Serikali kwa miaka kumi, akawa kivutio kikubwa kwa wafuasi wa upinzani katika kampeni za urais za mwaka 2015, na ambaye amepoteza mali na fursa za biashara kwa sababu za kisiasa.

Angetarajiwa awe lulu katika chama chochote cha siasa, tena akipewa nafasi kadhaa.

Angetarajiwa awe kivutio kwa mara nyingine katika uchaguzi mkuu ujao kama ilivyokuwa miaka minne iliyopita, lakini sasa atakuwa mwanachama wa kawaida baada ya kushindwa kupata kura za kumuwezesha kuwa mwenyekiti wa Kanda ya Pwani licha ya kusimama peke yake kugombea nafasi hiyo.

Kwa kuangalia boksi la kura, Sumaye ameshindwa kidemokrasia. Alipata kura 48 za “hapana” dhidi ya 28 za “ndiyo” licha ya Kamati Kuu kuengua wapinzani wake katika nafasi hiyo na kumbakiza peke yake na hivyo kuonekana kama angeshinda kirahisi.

Wanachama wa Chadema wamemuonyesha kuwa yeye ni mwanachama wa kawaida kama wengine.

Matokeo hayo yanaweza kumfanya Sumaye, ambaye tangu ahamie Chadema mwaka 2015 amekumbana na mikasa kama ya kunyang’angwa mashamba yake, ajiulize mara mbilimbili kama aendelee kubaki Chadema, arudi CCM kama wengine waliotoka chama hicho walivyofanya au apumzike siasa.

Lakini kuna dhana nyingi zinahusishwa na kuanguka ghafla kwa Sumaye katika uchaguzi wa viongozi wa Kanda ya Pwani, mojawapo na inayokuja kwa haraka ni kitendo chake cha kuchukua fomu ya kugombea uenyekiti ambao kwa takriban miaka 15 unashikiliwa na Freeman Mbowe.

Kwa namna moja, Sumaye anaona kuwa hiyo inaweza kuwa sababu na kwa namna nyingine anaona kushindwa kwake ni halali kwa kuwa alichotaka kufanya ni kuonyesha demokrasia imekomaaa ndani ya Chadema.

Baada ya matokeo, Sumaye alikiri kuwa ameadhibiwa kwa sababu ya kuchukua fomu za kutaka kuwania uenyekiti, ambao kwa baadhi ya wanachama kinaonekana kama usaliti na wengi wakiamini kuwa Mbowe, ambaye amekuwa mwenyekiti wa Chadema tangu mwaka 2004, bado anastahili kuendelea kuongoza chama hicho.

Lakini meya wa Ubungo, Boniface Jacob anasema kitendo hicho hakiwezi kuwa sababu ya Sumaye kuanguka.

“Kuna mambo mengi siwezi kuyazungumza kwa sababu sio msemaji wa chama. Ila itoshe kusema uchaguzi ni uchaguzi una matokeo mazuri na mabaya,” alisema Jacob alipoulizwa kuhusu Sumaye na uenyekiti.

“Mzee Sumaye bado anaheshimika ndani ya Chadema. Ila nimehuzunika na kauli yake kuwa ameadhibiwa kwa sababu ya kuchukua fomu ya uenyekiti.”

Katika mitandao ya kijamii, suala la Mbowe pia limehusishwa na njama za kushawishi wapigakura wamkatae Sumaye kuanzia ngazi ya kanda.

Imedaiwa kuwa mmoja wa viongozi wa Dar es Salaam alikusanya sehemu kubwa ya wapigakura na siku ya uchaguzi kwenda nao ukumbini, wakiwa wameshaweka msimamo mmoja wa kutompa kura waziri huyo mkuu wa zamani.

Na Meya Jacob ndiye anayelaumiwa zaidi na kwamba anaonekana kwenye video akishangilia kuanguka kwa Sumaye.

“Matokeo ya Sumaye yalitangazwa saa 8:00 mchana, ile video inayosambazwa ilichukuliwa saa 12:00 jioni wakati tukishangalia matokeo ya nafasi ya makamu mwenyekiti na mweka hazina. Hivi utasema nilikuwa nashangilia kushindwa kwa Sumaye?” anahoji Jacob, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

“Namheshimu Mzee Sumaye ndio maana nilitoa Sh70,000 kati ya 100,000 ikiwa ni sehemu ya mchango wa kumchukulia fomu ya kugombea nafasi hiyo. Leo utasemaje simpendi Sumaye na nafurahia yeye kushindwa uchaguzi?”

Alisema wanaosambaza hizo video na kumuunganisha yeye na tukio la Sumaye kushindwa uchaguzi hawana lengo zuri, kwa kuwa yeye ni miongoni mwa watu waliofanya ushawishi mkubwa kuhakikisha anagombea nafasi hiyo peke yake.

“Kwenye ile video utamuona Baraka Mwago na Mwita (meya wa Jiji la Dar es Salaam-waliogombea nafasi ya makamu mwenyekiti). Mwago ndiye aliyeshinda, lakini wote tulijumuika kusherehekea. Ndio desturi ya Chadema, sasa hapo utasema meya alikuwa anashangilia Sumaye kushindwa uchaguzi?” alihoji.

Maelezo ambayo Sumaye alitoa kuhusu kuanguka kwake ni kwamba nia yake ya kuwania uenyekiti wa Chadema-- nafasi inayoshikiliwa na Freeman Mbowe-- ndiyo iliyomuadhibu, lakini ataendelea kuwa mwanachama mtiifu.

“Ni kweli nimechukua fomu lakini sijaijaza wala kuirudisha kilichonishawishi kuchukua ni kutaka kuionyesha dunia ndani ya Chadema kuna demokrasia,” alisema Sumaye.

Dhana nyingine iliyotawala kuanguka kwa Sumaye ni demokrasia kushika hatamu.

Baada ya matokeo kutangazwa, Sumaye ambaye alikuwa mgombea pekee, alisema lililofanyika ni demokrasia ingawa hana uhakika kama kutoa adhabu kwa mtu aliyekuwa anatumia haki yake kufanya demokrasia ni sahihi.

Sumaye alisema alitaka kuionyesha dunia kuwa Chadema kuna demokrasia, lakini pengine chama hicho kimemuwahi na kuuonyesha ulimwengu kuwa yeyote anayetaka kumpinga Mbowe hawezi kuvumiliwa.

Suala la demokrasia kuchukua mkondo wake ndilo lililoelezwa na wengi waliohojiwa na Mwananchi kuhusu kuanguka kwa Sumaye.

“Wajumbe wa kikao husika ambao ni kikao cha kikatiba wa Chadema ndivyo walivyoamua kwa kura zao. Hicho ndivyo ninavyoweza kusema,” alisema Arcado Ntagazwa, mwenyekiti wa baraza la udhamini la Chadema.

“Kilichofanyika ni mchakato demokrasia si vinginevyo.”

Maoni kama hayo yalitolewa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala.

“Kwa mtu mzito kama Sumaye lazima kuwe na mshtuko, lakini hiyo ndiyo demokrasia,” alisema.

“Uamuzi umefanywa na wanachama au wajumbe na ndiyo demokrasia. Bila kujali yeye ni mkubwa kiasi gani.”

Alisema Chadema imeonyesha kukomaa kidemokrasia kwa kumpigia kura Sumaye aliyekuwa peke yake, kuliko wangemwacha kupita bila kupingwa.

“Hiyo ndiyo faida ya mgombea akiwa peke yake kupigiwa kura ya ndiyo au hapana ili wajumbe waamue hata kama yuko peke yake kama wanamtaka au hawamtaki.”

Alisema anashindwa kuunganisha kuanguka kwake na kuchukua fomu ya uenyekiti.

“Lakini ni kwamba kura zimepigwa maana yake ndiyo wameamua. Hayo mambo ya kupitisha mtu bila kupingwa si misingi ya demokrasia,” alisema Profesa Mpangala.

“Kama uchaguzi wa serikali za mitaa asilimia 99 wanasema wamepita wote bila kupigiwa kura za ndiyo au hapana. Je, wananchi wamewataka? Ilitakiwa kwamba mgombea akiwa peke yake wananchi wampigie kura. Siyo kupitisha watu kiholea.”

Kuna maswali mengi na mitazamo mingi imejitokeza. Je kitendo cha mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa aliyepata kura milioni sita na kuweka rekodi kwa wagombea urais wa vyama vya upinzani tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe, kumewafanya Chadema wasiwe na imani na watu waliojiunga na chama hicho kutokea CCM?

Lowassa, wabunge watatu, madiwani kadhaa na wenyeviti wa serikali za mitaa waliohamia chama hicho kutoka CCM, walitangaza kurejea walikotoka kwa vipindi tofauti, wengi wakieleza kuwa wanaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.

Lakini hiyo inaweza kuwa sababu dhaifu kwa sababu asilimia kubwa ya wanachama wa Chadema wamewahi kupita vyama vingine ikiwamo CCM.