Mto Congo unaweza kuzalisha megawati 100,000 za umeme – Utafiti

Tuesday November 5 2019

 

By Happiness Tesha, Mwananchi [email protected]

Kigoma. Watafiti wa Mto Congo unaozunguka nchi 10 za ukanda wa maziwa makuu, wamewasilisha tathmini ya utafiti wa awali wa miaka mitano wa mto huo ambao utawasaidia kupanga matumizi sahihi ya maji kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira.

Hayo yamebainishwa na mtafiti kiongozi,  profesa Preksedis Ndomba kutoka chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika kikao cha tathmini ya awali ya matokeo ya utafiti kwenye Mto Congo.

Kikao hicho kimefanyika jana Jumatatu Novemba 4, 2019  mjini Kigoma. Utafiti huo ulianza tangu mwaka 2016.

Profesa Ndomba amesema pamoja na mambo mengine, wameweza kubaini mto huo bado haujawekezwa vya kutosha.

Amesema Mto Congo unaopokea maji kutoka Ziwa Tanganyika, umebainika kuwa na rasilimali kubwa na una uwezo mkubwa wa kuzalisha megawati 100,000 za umeme, kiwango ambacho kinaweza kutatua changamoto ya tatizo la umeme kwa nchi nyingi barani Afrika.

“Pamoja na mambo mengine, tumeweza kubaini wananchi wanaozunguka ziwa hilo wanaweza kunufaika kwa kupata maji safi na salama, shughuli za kilimo pamoja na shuguli za kibiashara katika usafiri wa majini,” alisema Ndomba.

Advertisement

Awali, akifungua kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Kitila Mkumbo alisema Mto Congo una umuhimu mkubwa kwa ustawi wa nchi ya Tanzania na nchi zinazozunguka ziwa hilo.

Alisema utafiti huo ni muhimu kwao kwa sababu kina cha maji cha ziwa hilo kikipungua itakuwa ni hatari kwa maisha na uchumi wa wananchi wanazunguka ziwa hilo.

Mradi huo wa utafiti wa kutathmini Rasilimali maji katika Bonde la mto Congo kwa kuzingatia mahitaji na shughuli za maendeleo ya jamii.

Mradi huo unahusisha nchi 10 za Angola, Zambia, Tanzania, Burundi, Cameroon, Sudan kusini, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Jamhuri ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya kati na Rwanda.

Advertisement