VIDEO: Mtoto wa bilionea Msuya ashindwa kurejea kwenye nyumba ya baba yake, aitwa polisi

Mkuu wa wilaya ya Arumeru,Jerry Muro akiwa  mbele ya nyumba ya marehemu Bilionea Msuya akiwa amewakutanisha baba wa bilionea MsuyaErisaria Msuya,Mama Ndedhukuro Sikawa na mjukuu wao,Kelvin Msuya ambao kwa muda mrefu walikuwa hawazungumza,baada ya kuagiza warejeshwe watoto katika nyumba ya wazazi wao. Picha Mussa Juma

Muktasari:

Bilionea Erasto Msuya alifariki baada ya kupigwa risasi Agosti 7, 2013 katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai mkoani Kilimanjaro akiwa kwenye biashara ya kuuza madini ya Tanzanite.

Arusha. Licha ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha nchini Tanzania, Jerry Muro jana Alhamisi kuagiza watoto wa marehemu bilionea Erasto Msuya kurejea katika  makazi ya baba yao katika nyumba ya kifahari iliyopo eneo la Sakina katika jiji la Arusha lakini imeshindikana.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Oktoba 18, 2019, Kelvin Msuya(22) ambaye ni mtoto mkubwa wa Msuya alisema ameshindwa kurejea katika makazi yao kutokana na kutokamilika kwa masuala ya kisheria baada ya kuitwa polisi kutoa maelezo na kubainika nyumba hiyo ni sehemu ya mali ambazo zimeandikwa na bibi yake, Ndeshekuru  Sikawa katika kesi ya mirathi.

“Leo tangu asubuhi tuliitwa polisi kutoa maelezo ya mgogoro huu, sasa inavyoonekana kuna maswala ya kisheria bado serikali inafanya ili kuhakikisha tunapata haki yetu,” amesema

Kelvin amesema wito huo wa polisi ulitokana na maagizo ya Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambaye pia ametaka suala hilo kushughulikiwa na kumalizwa kwa amani na utulivu.

“Hivyo, nimeona kwa kuwa pia Jumatatu tuna kikao na ndugu wa baba tunaweza kukamilisha baadhi ya mambo ili hata nikirejea katika makazi niishi kwa amani,” amesema

Amesema kwa sasa kwa kuwa yupo peke yake hapa nchini, wadogo zake wawili bado wapo shule Nairobi nchini Kenya.

Hata hivyo, Kelvin ameiomba pia Serikali ya Tanzania kusaidia kesi ambayo inamkabili mama yake, kusikilizwa kwani ndugu hao wa baba yake wamekuwa wakiweka mapingamizi ambayo yanalenga kucheleweshwa kesi hiyo.

Juzi, Gambo alikutana na mtoto huyo na mjomba wake ambapo aliagiza ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali kufuatilia jambo hili.

Nyumba hiyo waliorejeshewa watoto kuishi ni kati ya nyumba tano za bilionea huyo, zilizokuwa zimefungwa  na ndugu wa bilionea huyo, kwa kile walichoeleza sababu za kiusalama na zipo katika  kesi ya mpya ya kuomba usimamizi wa  Mirathi, iliyofunguliwa na mama wa Msuya, Ndeshukuru Sikawa.

Muro  alisema sambamba na kuwarejesha watoto katika nyumba hiyo, amewataka wawakilishi wa familia ya Msuya na Mke wa bilionea huyo, Miriam Mrita  kukutana ofisini kwake Jumatatu Oktoba 21, 2019 ili kuzungumzia muafaka wa mgogoro huo.

Miriam  anashikiliwa katika gereza la Segerea  Dar es Salaam kwa tuhuma za kesi ya mauaji ya dada wa bilionea huyu, Aneth Msuya, mauaji yaliyotokea Kigambanoni jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, dada wa bilionea huyo, Upendo Msuya alisema wao kama wanafamilia hawana nia ya kudhulumu bali ya watoto bali walifunga nyumba kwa sababu za kiusalama baada ya kuona ndugu wa mke wa marehemu wakichukua vitu.

“Wakati tunafunga nyumba huyu Kelvin alikuwa anasoma Australia na wadogo zake Nairobi hivyo kwa sababu wamerudi hatuna tatizo kwani tunajua sisi sio wamiliki wa nyumba hizi,” alisema

Bilionea Msuya ameacha nyumba za kifahari tano, viwanja maeneo mbali mbali nchini, hoteli mbili za kitalii SG resort na Mezaruna, magari na mali nyingine mbalimbali.