Mtoto wa kwanza wa Sokoine kuzikwa Jumanne Monduli Juu

Hii ndiyo picha halisi ya Lazaro Sokoine, tofauti na ile iliyotumika katika taarifa zetu zilizotangulia. Tunaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza.

Mhariri

Arusha. Lazaro Sokoine, mtoto wa kwanza wa Waziri Mkuu wa zamani Edward Moringe Sokoine aliyefariki dunia Jumamosi Machi 28, 2020 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili atazikwa Jumanne Machi 31 Monduli Juu mkoani Arusha.

Msemaji wa familia ya Sokoine, Namelock Sokoine amesema mwili wa marehemu Lazaro utasafirishwa Jumatatu Machi 30 kwenda Monduli na mazishi yatakayofanyika Jumanne nyumbani kwao Monduli Juu.

Kuhusu kifo chake, Kaka yake marehemu, Balozi Joseph Sokoine amesema Lazaro alianza kutibiwa maumivu ya kifua katika Hospitali ya Rufaa Morogoro kabla ya kuhamishiwa Muhimbili ambako mauti yamemkuta.

"Aliugua kifua kwa muda mrefu...pafu moja liliharibika na kushindwa kufanya kazi kabisa," alisema Balozi Sokoine.

Lazaro ni miongoni mwa watoto 11 wa Marehemu Edward Sokoine, sita wa mke mkubwa, Napono; na watano wa mke mdogo, Nekiteto.

Lazaro aliyekuwa anaishi Morogoro kwa shughuli zake za kijasiriamali, alizaliwa Enguiki, Monduli - Arusha Machi 13, 1961 na ameacha watoto wawili.