Mtoto wa miaka 15 kupima VVU bila ridhaa ya mzazi

Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu(kulia) akizungumza na Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia wakati wa Mkutano wa Kumi na saba kikao cha saba bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Bunge limepitisha marekebisho ya  Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa VVU na Ukimwi yanayoruhusu umri wa kupima virusi vya ugonjwa huo bila ridhaa ya mzazi au mlezi kuwa miaka 15.

Dodoma. Bunge limepitisha marekebisho ya  Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa VVU na Ukimwi yanayoruhusu umri wa kupima virusi vya ugonjwa huo bila ridhaa ya mzazi au mlezi kuwa miaka 15.

Sheria  hiyo ipo katika muswada wa Sheria ya Marekebisho Mbalimbali namba saba wa mwaka 2019 uliowasilishwa na kupitishwa na Bunge leo Jumanne Novemba 12, 2019.

Katika mjadala wa muswada huo hoja kubwa ilikuwa umri wa mtoto kuruhusiwa kupima bila ridhaa ya mzazi ama mlezi huku Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ikitaka umri huo kushushwa hadi miaka 12. Kabla ya mabadiliko hayo umri wa kupima bila ridhaa ya mzazi ulikuwa miaka 18.

Akizungumza bungeni mjini Dodoma Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amesema lengo la kupeleka marekebisho hayo  ni kuongeza kasi ya upimaji.

Alibainisha kuwa lengo ni kutokomeza ugonjwa wa Ukimwi hadi ifikapo mwaka 2030,  na kwamba kinachosumbua ni lengo la kwanza la upimaji wa VVU kufikia asilimia 90 na kuondokana na hali ilivyo sasa ya asilimia 62.

Amesema hoja kubwa iliyoletwa na Kambi Rasmi ya ya Upinzani kuhusu marekebisho hayo ni umri wa kujipima mtoto ushuke hadi miaka 12.

“Haikatazwi kwa mtoto kupima VVU akiwa chini ya miaka 15 lakini bado ni msimamo wa Serikali apime kwa ridhaa ya wazazi tusitake kuiga tu mambo,” amesema.

Amesema wanao ushahidi wa kitakwimu kuwa kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watoto wa chini ya miaka 14 ni asilimia  0.4.

“Sasa hawa mnasema wakajipime bila ridhaa ya wazazi,” amehoji.

Amesema kwa umri huo maambukizi mengi ni ya  kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Pia amesema takwimu zinaonyesha umri wa mihemuko ya watoto kufanya mapenzi ni miaka 15.