Mufti atoa salamu za pole ajali ya moto iliyoua 69 mkoani Morogoro

Muktasari:

  • Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir ametoa salama za rambirambi kwa Rais John Magufuli na Watanzania wote kwa kupoteza wapendwa wao katika ajali ya moto iliyotokea jana mkoani Morogoro na kusababisha vifo vya watu 69 hadi leo Jumapili Agosti 11, 2019 saa 5 asubuhi

Dar es Salaam. Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir ametoa salama za rambirambi kwa Rais John Magufuli na Watanzania wote kwa kupoteza wapendwa wao katika ajali ya moto iliyotokea jana mkoani Morogoro na kusababisha vifo vya watu 69 hadi leo Jumapili Agosti 11, 2019 saa 5 asubuhi.

"Nimepokea kwa masikitiko taarifa za msiba huko Morogoro baada ya lori la mafuta kulipuka. Natoa pole kwa Rais Magufuli kwa kuondokewa na nguvu kazi ya Taifa, pia natoa pole kwa watoto wote kwa kuondokewa na wazazi na walezi wao," amesema Mufti.

Amewaagiza viongozi wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) mkoani Morogoro kutoa ushirikiano utakaohitajika katika kipindi hiki cha msiba.

Ajali hiyo imetokea jana Jumamosi Agosti 10, 2019 mita 200 kabla ya kufika stendi ya mabasi ya Msamvu barabara ya Morogoro-Dar es Salaam  baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta hayo imehifadhiwa mochwari.

Wakati huo huo, Mufti amesema sherehe za sikukuu ya Iddi zitafanyika kesho Agosti 12, 2019  na swala ya Iddi kitaifa itafanyika katika msikiti wa Masjidi Kibadeni uliopo Chanika jijini Dar es Salaam na Baraza la Iddi litafanyika hapo pia.

Amesema mgeni rasmi kwenye swala ya Iddi atakuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo. Amewataka Waislamu kusherehekea kwa amani na utulivu bila kukiuka misingi ya Mwenyezi Mungu.