Museveni azungumzia siri ya kushinda urais

Muktasari:

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema si rahisi kwa mgombea urais kuibuka na ushindi katika nchi za Bara la Afrika  bila kuwa mwanachama wa chama cha siasa chenye mwelekeo mzuri.

 

Dar es Salaam. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema si rahisi kwa mgombea urais kuibuka na ushindi katika nchi za Bara la Afrika  bila kuwa mwanachama wa chama cha siasa chenye mwelekeo mzuri.

Ameeleza hayo leo Alhamisi Novemba 5, 2020 wakati akizungumza katika hafla ya kuapishwa kwa Rais wa Tanzania, John Magufuli. Magufuli ameapishwa kuwa rais wa Tanzania kwa mhula wa pili.

“Hayati mzee wetu Daniel Arap Moi alitukumbusha neno moja  la kufuata nyayo za kisiasa za marehemu Jomo Kenyata, sifuatilii Tanzania hapa lakini wakati wa uchaguzi najikuta naweka TV yenu hapa inaitwa TBC1 naanza kutazama kuona huu uchaguzi unakwenda vipi nadhani sababu ni kwamba najua mwelekeo wa CCM kisiasa hivi vyama vingine sijui mwelekeo wao.”

“Wengine wanafikiri ni jambo rahisi, lakini Afrika kufaulu lazima tukumbuke hilo jambo la mwelekeo wa kisiasa, baada ya uhuru viongozi wetu waligawanyika,  wengi wa Afrika walichukua mstari wa kuwa vibaraka wa nchi za nje wachache wakiongozwa na mwalimu Nyerere (Julius- Rais wa kwanza wa Tanzania) na wengine kama kina Mzee Kaunda na Seretse Khama walikataa,” amesema Museveni.

Ameongeza, “kama tungefuata mstari ule mwingine wa vibaraka hawa viongozi hawangekuwa hapa,  Kusini ya Afrika yote ilikuwa chini ya wakoloni kwa hiyo mnisamehe kuwa natazama TBC 1 kujua inakwendaje uchaguzi wa 2015 nilikuwa na hofu sana hii imekuwaje? Lakini baadaye nikaona alichaguliwa kwa kura nyingi sana.”

“Safari hii nikaona tena kule Hai nikasema heee Hai, hata Ilemela haya ndiyo majimbo ambayo walitangaza kwanza Newala huko nikasema aah basi, sasa mwisho naona nikiangalia umati wa watu hapa naona vijana wengi sana lakini vijana lazima mrithi msimamo wa wazalendo ambao walitangulia wakiongozwa na Mwalimu Nyerere.”

Museveni amesema yeye amekuwa mfuasi wa Nyerere kwa miaka 57 na hajawahi kumwangukia yeyote na mambo yaliyolengwa yalikuwa manne pekee.

“Kwanza ukombozi wa Afrika yote, pili ustawi na hii haiwezi kutoka kwenye kuomba kila siku inatokana na uzalishaji mali ya bidhaa na huduma, tatu ni ulinzi makini kwa Afrika na undugu. Sisi wafuasi wa Mwalimu Nyerere kutoka nyuma haya ndiyo mambo yetu manne,” amesema Museveni.

Amempongeza Rais Magufuli na chama chake cha CCM kwa kupata ushindi wa kishindo.