Mvua kunyesha wastani wa juu Dar, Pwani

Dar es Salaam.Mamlaka ya Hewa Tanzania(TMA) imesema mabadiliko makubwa yanayoendelea katika Bahari ya Hindi na baadhi ya maeneo ya misitu ya Congo imesababisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro Kaskazini  kutarajiwa kunyesha mvua juu ya wastani.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi amesema hayo leo Jumatano Aprili 8 wakati akitoa ripoti ya tathmini ya hali ya hewa nchini ya mwaka 2019.

Amesema katika mifumo ya hali ya hewa kuna mabadiliko yanaendelea katika Bahari ya Hindi na baadhi ya maeneo ya misitu ya Congo ambayo yanasababisha  mikoa hiyo kupata mvua  wastani hadi juu ya wastani.

Pia amesema eneo kubwa la Kaskazini mwa nchi litapata mvua wastani hadi juu ya wastani isipokuwa eneo la Magharibi mwa Ziwa Victoria ambapo itapata mvua wastani hadi chini ya wastani.

"Mvua hizi zimeshaanza kunyesha na maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka inatarajiwa mvua hizo kuisha Aprili na maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka zitaisha Mei wiki ya pili na ya tatu," amesema Dk Kijazi

Dk Kijazi amesema  sekta mbalimbali wanaotumia taarifa hizo kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya nchi wanatakiwa kufuatilia ili waweze kuchukua hatua.