Mvua yapaisha bei ya nyanya

Monday December 30 2019

Baadhi ya wachuuzi wa nyanya wakizikagua katika

Baadhi ya wachuuzi wa nyanya wakizikagua katika soko la Sterio 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini imesababisha kupanda kwa bei ya nyanya katika jiji la Dar es Salaam.

Mwananchi imefika katika baadhi ya maeneo leo Jumatatu ya Desemba 30, 2019 ili kuangalia upatikanaji wa nyanya na kukuta nyingi zinazouzwa ni zile zilizoanza kuharibika.

Akizungumza na Mwananchi leo saa Tano asubuhi, muuzaji wa nyanya kwa bei ya jumla katika soko la Sterio wilayani Temeke, Khamis Kadogo amesema mvua zinazonyesha katika maeneo ya mashambani imesababisha kuharibika kwa nyanya.

“Nyingi zilizokuwa zimeiva zinapasuka kutokana na kujaa maji nyingine zinabebwa  hivyo shambani zinabaki chache jambo ambalo linafanya na wao kupandisha bei,” amesema Kadogo.

Amesema nyanya nyingi zinazouzwa leo katika soko hilo ni zile ambazo haziwezi kustahimili kukaa kwa siku tatu jambo ambalo linaweka ugumu kwa wachuuzi wadogo kuzinunua kwa sababu zinaweza kuwapa hasara.

“Tunaziuza kati ya Sh48,000 hadi Sh40,000 ambazo ni angalau ngumu zile zilizoharibika zaidi ambazo endapo mtu akitaka kununua labda azitumie zote ziishe, bei yake inafika Sh30,000 kwa boksi moja.”

Advertisement

“Bei imeshuka sana leo kwa sababu zimeingia nyanya nyingi lakini juzi boksi moja la nyanya liliuzwa kati ya Sh70,000 hadi Sh80,000,” amesema Kadogo.

Ramadhan Seif ambaye pia ni muuzaji wa jumla, amesema licha ya kuwa mvua inabeba nyanya mashambani, lakini pia huweka ugumu kwa magari kufika katika mashamba hayo kubeba mzigo.

“Matope, utelezi wengi wanagoma na hata wakikubali bei inakuwa kubwa sana jambo ambalo linafanya wengi kukata tamaa ya kuchukua mzigo kwa sababu wanaweza wasipate faida.”

Wakati wanunuzi hao wa jumla wakipandisha bei ya boksi hali imekuwa sawa na wale wadogo ambao huuza kwa sado katika soko hilo.

Baadhi wanauza sado kwa Sh10,000 hadi Sh9,000 huku wengine wakiuza kwa Sh6,000 hadi Sh7,500 na sado ndogo zikiuzwa kati ya Sh5,000, Sh4,500 na Sh3,000.

“Dada hizi nyanya nakuuzia kwa Sh10,000 kwa sababu ni nzuri ngumu na haiharibiki hata ikae siku ngapi huwezi kujutia uamuzi wako,” alisema muuzaji wa nyanya hizo aliyejitambulisha kwa jina moja la Fred.

Mariam Jau amesema anauza sado ya nyanya kwa Sh6,000 kwa sababu siyo kavu “Nikisema kavu na maanisha ambazo ni nzima kabisa hazina majeraha hizi zangu zimejaa maji kutokana na mvua huko mashambani zikikaa muda mrefu zitaharibika.”

Lakini wakati hali ikiwa hivyo katika soko hilo, mtaani nyanya moja inauzwa kwa kati ya Sh150 hadi Sh300.

Mmoja wa wauzaji wa nyanya kwa rejareha katika eneo la Mtoni Kijichi, Maria Babu amesema mara nyingi wao hupandisha bei kulingana na bei ya jumla wanayonunulia.

“Juzi tulinunua nyanya kwa Sh70,000 tungeuza shilingi ngapi ili tupate na faida, basi tu tunauza kwa sababu ni biashara ambayo tumeizoea na hatuwezi kuiacha,” amesema Maria.

Advertisement