VIDEO: Mvua yasababisha mafuriko Tandale, Jangwani

Muktasari:

  • Mvua iliyonyesha jana usiku na asubuhi ya leo imesababisha mafuriko kwa wakazi wa Tandale na Jangwani jijini Dar es Salaam. Maji yamejaa kwenye makazi yao na kusababisha foleni kwenye barabara zinazopita maeneo hayo.

Dar es Salaam. Wakazi wa Tandale jijini Dar es Salaam wamekumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua iliyoanza kunyesha usiku wa kuamkia leo na kusababisha makazi yao kujaa maji.

Wananchi hao wamesema mafuriko hayo yamesababishwa na ujenzi wa barabara ya Tandale kwa sababu mifereji yake ni midogo na imefunikwa tofauti na iliyokuwapo kabla ambayo ilikuwa wazi ikiruhusu maji kuingia moja kwa moja.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Machi 3, 2019, mkazi wa Tandale, Ibrahim Simba amesema tatizo limeongezeka baada ya barabara hiyo kujengwa ikiwa na mifereji iliyofunikwa na ni midogo.

“Tunafurahi kujengewa barabara, lakini ndiyo imeongeza tatizo huku Tandale, mifereji yote imejaa maji, sasa maji yanatokea kwenye matundu ya kupumulia na kujaa kwenye nyumba zetu," amesema Simba.

 

Mkazi mwingine wa Tandale, Sina Chaurembo amesema mafuriko yalikuwepo hata siku za nyuma lakini sasa yameongezeka baada ya barabara kuinuliwa juu, hivyo maji yanashuka kwa urahisi kwenye makazi ya watu.

"Kama unavyoona, maji yamejaa kwenye mifereji, kwa hiyo yanatafuta upenyo na kutokea juu au ubavuni. Tunaomba mkandarasi abadilishe muundo wa hii mifereji, tuliwashauri lakini wakasema hayo ndiyo maelekezo waliyopewa.

Mwananchi Digital imetembelea pia eneo la Jangwani na kujionea Mto Msimbazi ukiwa umejaa. Baadhi ya makazi ya wananchi pia yamekumbwa na mafuriko hayo huku wananchi wakilalamikia mfereji wa TBL.

"Haya maji yanasababishwa na ule mfereji wa Breweries. Mfereji umejaa mchanga, kwa hiyo maji yanakuwa juu na yanachepuka kirahisi kuja huku kwetu. Ule mfereji ungekuwa umechimbwa, maji hayawezi kufika huku," amesema Edward Mali, mkazi wa Jangwani.

Maji yamefurika pia katika daraja la Jangwani na kusababisha maji kuelekea kwenye jengo la kuegesha magari yaendayo haraka (UdaRT).

Mwananchi Digital imeshuhudia mabasi yakitumia geti la nyuma kuingia na kutoka kwenye maegesho hayo.