Mvua yaua mmoja Dar es Salaam

Muktasari:

Mvua ambazo zimeanza kunyesha tangu asubuhi leo Alhamisi jijini Dar es Salaam nchini Tanzania imesababisha adha ya usafiri na kifo cha mtu mmoja.


Dar es Salaam. Mvua iliyonyesha leo Alhamisi Novemba 21, 2019 jijini Dar es Salaam nchini Tanzania imesababisha kifo cha Mwenga Agustino mwenye umri wa miaka 78 katika mtaa wa Stakishari.

Inaelezwa kutokana na maji yaliyokuwa yamezidi katika eneo hilo, Agustino alikuwa akifanya jitihada za kujiokoa kutoka ndani kwake baada ya maji kujaa.

Mzee huyo wakati anafana jitihada za kutoka ndani maji yalimzidi na licha ya wananchi kumuokoa na kumkimbiza Hospitali ya Amana, jitihada hizo hazikuzaa matunda kwani alifikwa na mauti kabla hajafika.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Shina la Stakishari, Majaliwa Saady alithibitisha kutokea kwa kifo hicho ambacho kimesababishwa na maji baada ya kukosa njia ya kutokea.

"Kweli mzee wetu hapa mtaani amekufa kutokana na maji ambayo yamejaa, haya maji yametokana na ujenzi wa Merkezi kuzuia maji yasipate njia ya kutoka," alisema.

Wananchi baada ya kuona maji yanaendelea kushuka mtaani kwao, walibidi watumie njia mbadala ya kuvunja ukuta wa mtu ili kuweza kupitisha maji hayo.

Mwananchi lilishuhudia tukio hilo na baadaye walikuja Askari wa Zimamoto (Fire) kwaajili ya kuangalia maafa ambayo yamejitokeza ili kuweza kutoa msaada.