Mwakilishi ACT-Wazalendo kuzikwa leo jioni

Muktasari:

Mwili wa aliyekuwa mwakilishi mteule wa  Pandani Pemba kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Abubakar Khamis Bakar utazikwa leo jioni Jumatano Novemba 11, 2020 saa  10 jioni katika makaburi ya Kianga yaliyopo Mbweni Unguja.

Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa mwakilishi mteule wa  Pandani Pemba kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Abubakar Khamis Bakar utazikwa leo jioni Jumatano Novemba 11, 2020 saa  10 jioni katika makaburi ya Kianga yaliyopo Mbweni Unguja.

Bakar ambaye amewahi kuwa waziri wa katiba na sheria katika Serikali ya Umoja ya Kitaifa (SUK) kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 amefariki dunia ghafla usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake  Mbweni.

Mwakilishi licha ya kuibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 alikuwa bado hajakula kiapo katika baraza la wawakilishi linalozinduliwa leo na Dk Mwinyi.

Kwa mujibu wa Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter, amesema hadi umauti unamkuta Bakar alikuwa mjumbe wa kamati kuu  pamoja na mwenyekiti wa kamati ya maadili ya chama hicho.

“Kwa uchungu mkubwa nawajulisha kuhusu msiba mkubwa tulioupata wa mjumbe wa kamati kuu ya chama na mwenyekiti wa kamati ya maadili Abubakar Khamis Bakar.”

“Mitihani naibu katibu mkuu wa chama Nassor Mazrui siku ya 14 ameshikiliwa bila kupelekwa mahakamani, mjumbe wa kamati kuu Ismail Jussa  jana kafanyiwa upasuaji mwingine Nairobi. Mjumbe wa kamati kuu Abubakar ametangulia mbele ya haki, Allah atatuvusha inshallah,” ameandika Zitto.

Mazrui na wenzake 32 walikamatwa na polisi Oktoba 28, 2020 wakidaiwa kukutwa na vifaa vya kuingilia mfumo wa matokeo, hata hivyo baadhi yao waliachiliwa lakini naibu katibu mkuu huyo na wenzake saba walisafirishwa hadi Dar es Salaam.