Mwalimu aahidi kumpa Bashe ukuu wa wilaya

Mgombea Mwenza wa Urais  Chadema Salum Mwalimu akimnadi mgombea ubunge wa Chama chake katika jimbo la Nzega Mjini Mary Atonga

Muktasari:

Mgombea mwenza wa Chadema, Salum Mwalimu amesema atafikiria kumpa ukuu wa wilaya mgombea ubunge wa CCM Nzega mjini, Hussein Bashe ikiwa atakubali kumuachia jimbo hilo mgombea wa Chadema, Mary Atonga.

 

Nzega. Mgombea mwenza wa Chadema, Salum Mwalimu amesema atafikiria kumpa ukuu wa wilaya mgombea ubunge wa CCM Nzega mjini, Hussein Bashe ikiwa atakubali kumuachia jimbo hilo mgombea wa Chadema, Mary Atonga.

Mwalimu ameeleza hayo leo Jumamosi Oktoba 24, 2020 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Nzega mjini mkoani Tabora.

Mwalimu amesema Bashe ni rafiki na kaka yake hawezi kumsahau akiwa Ikulu baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28,2020 endapo Chadema kitashika Dola.

"Nasikia kaka yangu Bashe naye ana mkutano leo kwenye kata hii na ana mechi ya mpira haya sawa tu, hamna shida mimi nilidhani kuwa angeonyesha onyesha nidhamu ili walau baada ya tarehe 28 nimkumbuke hata kwenye ukuu wa wilaya maana ni rafiki yangu, ni kaka yangu sasa ananionyesha utovu wa nidhamu makamu wa Rais," amesema Mwalimu.

Huku akishangiliwa na wananchi, Mwalimu aliwataka  wakazi wa eneo hilo kumfikishia salamu Bashe ambaye ni naibu waziri wa Kilimo.

Amesisitiza  kuwa licha ya kile alichodai ni utovu wa nidhamu wa Bashe kufanya mkutano siku moja na wake, atamfikiria kwenye ukuu wa wilaya ila ubunge amuachie Mary.