Mwalimu atumia kitenge cha mkewe kujinyonga, mjasiriamali akutwa akining’inia

Kamanda wa Polisi Mkoani Tabora, Barnabas Mwakalukwa

Muktasari:

  • Polisi mkoani Tabora nchini Tanzania inaendelea na uchunguzi matukio mawili ya wanaodaiwa kujinyonga kwa nyakati tofauti.

Tabora. Mwalimu Basil Sungu (39) wa shule ya msingi Ikongolo Wilaya ya Uyui mkoani Tabora nchini Tanzania amejinyonga hadi kufa kwa kutumia kipande cha kitenge cha mke wake.

Kamanda wa Polisi Mkoani Tabora, Barnabas Mwakalukwa amesema mwili wa Sungu ulikutwa chumbani kwake ukiwa umening’inia darini Jumanne iliyopita ya Desemba 31, 2019.

“Uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea ingawa taarifa za awali zinadai kabla ya kifo chake, marehemu alikuwa na mgogoro wa kifamilia na mke wake Theresia Ali,” amesema Kamanda Mwakalukwa

Katika tukio lingine, Kamanda huyo wa polisi amesema James Albert (22), mjasiriamali na mkazi wa kata ya Chemchem Manispaa ya Tabora amekutwa amejinyonga hadi kufa kwa kutumia mkanda wa begi.

Amesema polisi wanaendelea na upelelezi kubaini kwanini marehemu aliyekutwa akining’inia kwenye kenchi za paa sebuleni kwake kuchukua uamuzi wa kujitoa uhai.