Mwambe amwakilisha Mbowe msiba Mbunge CCM

Muktasari:

Mbunge wa Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe amemuwakilisha kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani, Freeman Mbowe bungeni na kusema walipokea taarifa za kifo kwa mshtuko na yeye amepoteza mbunge jirani ambaye wamepakana.

Newala. Mbunge wa Ndanda (Chadema) nchini Tanzania, Cecil Mwambe amemuwakilisha kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe katika mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Newala vijijini (CCM), Rashid Akbar akisema kifo cha mbunge huyo ni kipo kubwa.

Akbar aliyefariki jana Jumatano Januari 15, 2020 akiwa Mkoa wa Lindi amezikwa leo Alhamisi  mkoani humo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Bunge na wananchi wa ndani na nje ya Newala.

Akizungumza wakati wa kutoa salamu kwa niaba ya kambi ya upinzani bungeni, Mwambe amesema walifanya kazi na Akbar kama mbunge mwenzao na walipokea taarifa za kifo chake kwa mshtuko na huzini.

Mwambe amesema mbali na kuwa mbunge mwenzao lakini amepoteza mbunge jirani wa jimbo kwani wanapakana na hata wananchi wao wanategemeana katika baadhi ya huduma kama barabara na afya.

“Nimesimama kwa niaba ya kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, mheshimiwa Akbar tumefanya naye kazi kwa takribani miaka minne na tunafahamu ufanyaji wake wa kazi, tumepokea taarifa za kifo chake kwa kushtuka na kwa huzuni kubwa kwa hiyo  na sisi tukasema tuje tushiriki na kueleza wananchi wa Newala vijijini kwamba tumepata pigo,” amesema Mwambe

“Tunafanya wote kazi za siasa lakini tunaunganishwa na imani yetu kwamba kwa lengo moja tuna nia ya kujenga nchi yetu, kwa hiyo tofauti zetu za kisiasa zisitufanye sisi tukawa tofauti kwenye kutekeleza majukumu yetu ya kuijenga nchi yetu,” amesema Mwambe

Amesema namna nyingine alikuwa karibu kwani ni wabunge majirani wa jimbo la Ndanda na Newala vijijini.

“Kulikuwa na mambo mengi yanayotuunganisha kwanza matibabu kwa maana ya hospitali ya Ndanda na barabara inayounganisha wilaya ya Masasi na Newala kupitia Miyuyu, tulifanya wote juhudi kwa pamoja na nina amini kazi zinaonekana,” amesema Mwambe

Marehemu Akbar alizaliwa Januari 25,1961, ameacha mke mmoja na watoto wanne.