Mwanafunzi apigwa risasi akiingia Ikulu Kenya

Muktasari:

Alikamatwa na polisi kwa kuingia Ikulu ya Nairobi kinyume cha sheria


Nairobi, Kenya. Mwanafunzi wa chuo kikuu anayesomea taaluma ya uhandisi amekamatwa akidaiwa kuingia Ikulu kinyume cha sheria.

Brian Bera (25) ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) alikamatwa na polisi kwa kuingia Ikulu ya Nairobi kinyume cha sheria.

Gazeti la Taifa Leo limeripoti kuwa mwanafunzi huyo, ambaye alipanda lango moja la Ikulu, alipigwa risasi na polisi wanaolinda kwenye lango hilo baada ya kuchomoa kisu alipotakiwa asimame.

Tukio hilo lilisababisha mwanafunzi huyo kuumia katika bega la kushoto.

Tukio hilo linadaiwa kutokea jana Jumatatu saa 10:15 jioni na mtuhumiwa alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kileleshwa kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) kwa matibabu.

Uchunguzi unaendelea kubainisha nia yake ya kuingia Ikulu kinyume cha sheria na hatua zifaazo zitachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika.

Taarifa iliyotolewa jana na Ikulu iliwakumbusha wananchi wa Kenya kwamba Ikulu ni sehemu iliyotengwa kuwa chini ya ulinzi mkali kwa mujibu wa Sheria ya Maeneo Yanayolindwa.

“Kwa sababu hiyo, hakuna yeyote anaruhusiwa kuingia Ikulu pasipo na ruhusa kutoka kwa asasi ama maafisa waliotwikwa mamlaka jukumu hilo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.