Mwanajeshi aua watu 26 kwa risasi, mwenyewe auawa

Muktasari:

Imetokea nchini Thailand na waziri mkuu wa nchi hiyo amesema na mwanajeshi huyo ni miongoni mwa waliouawa.

Bangkok. Takriban watu 27 wamefariki baada ya kupigwa risasi kiholela na mwanajeshi mmoja wa Thai katika mji wa Nakhon Ratchasima, maafisa wa polisi wamesema.
Msemaji wa wizara ya ulinzi amesema kwamba mwanajeshi huyo, Jakraphanath Thomma, mwenye cheo cha chini alimshambulia mkuu wake kabla ya kuiba bunduki na risasi kutoka katika kambi ya kijeshi.
Baadaye aliwafyatulia risasi waumini waliokuwa katika hekalu na duka la jumla katika mji huo.
Picha zilizochapishwa katika mitandao ya kijamii zimekuwa zikionyesha eneo ambalo shambulio hilo la risasi limefanyika karibu na duka la jumla.
Picha za vyombo vya habari zinaonekana zikionyesha mwanajeshi huyo akitoka katika gari moja na kuwafyatulia watu risasi kiholela.
Picha nyengine zilionyesha moto nje ya jengo hilo, huku kukiwa na ripoti kwamba ulisababishwa na gesi iliolipuka baada ya kupigwa risasi.
"Mwanajeshi huyo alitumia bunduki ya kivita kuwapiga risasi watu wasio na hatia na kuwajeruhi wengi huku wengine wakifariki,” msemaji wa serikali Krissana Pattanacharoen amesema.
Baada ya kurushiana risasi na hali ya kutisha usiku kucha, wadunguaji walifanikiwa kumuua mwanajeshi huyo leo Jumapili asubuhi.
Kwa ujumla watu 26 wakiwamo raia, mdogo akiwa mvulana wa miaka 13, na wanajeshi waliuawa katika tukio hilo,” waziri Mkuu wa Thailand, Prayut Chan-O-Cha ameileza AFP.
Hali ikoje hivi sasa?
Mapema, mamlaka imelizunguka eneo alikokuwa mshambuliaji huyo huku ikijaribu kumtafuta.
Polisi iliwaonya raia kusalia majumbani mwao, gazeti la Bangkok Post limeripoti kwamba mhusika mwenye umri wa miaka 32 amejificha alikuwa ndani ya jumba hilo.
Sauti zaidi za risasi zimesikika ndani ya jumba hilo.
Atuma ujumbe
Wakati akiendelea kusakwa mwanajeshi huyo alituma ujumbe katika mtandao wake akiuliza iwapo ajisalimishe.
Awali, alikuwa amechapisha picha ya bastola na risasi tatu, pamoja na maneno “ni wakati wa kujifurahisha” na hakuna mtu anayeweza kuzuia kifo”.
Ukurasa wake wa facebook baadaye umeondolewa.
Gazeti la Bangkok Post limesema kamanda aliyeshambuliwa na mshukiwa huyo hadi kufa ni Kanali Anantharot Krasae na kwamba mwanamke mwenye umri wa miaka 63 na mwanajeshi mwingine waliuawa katika kambi hiyo.