Mwanamke aliwa na mamba

Muktasari:

Rulensi Igayo (28) mkazi wa kijiji cha Kisaba kata ya Maisome halmashauri ya Buchosa Mkoa wa Mwanza amekufa baada ya kuliwa na mamba wakati akiogelea katika ziwa Victoria.

Buchosa. Rulensi Igayo (28) mkazi wa kijiji cha Kisaba kata ya Maisome halmashauri ya Buchosa Mkoa wa Mwanza amekufa baada ya kuliwa na mamba wakati akiogelea katika ziwa Victoria.

Mkuu wa wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole amethibitisha kifo hicho na kuwataka wananchi kuacha tabia ya kuoga ziwani, akishauri wachote maji na kwenda kuoga majumbani mwao.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kisaba amesema tukio hilo limetokea leo Jumamosi Oktoba 24, 2020 saa 12 alfajiri baada ya Rulensi  kwenda katika ziwa hilo kuoga.

Amesema taarifa za mwanamke huyo kuliwa na mamba zilitolewa na mvuvi aliyetambulika kwa jina moja la Charles aliyekuwa akienda kuvua samaki, alipofika eneo hilo alikuta nguo za Rulensi na alipotazama kwenye maji alimuona mamba akiibuka na kuzama mdomoni akiwa na mwili wa mwanamke huyo.

Yahaya amesema kwa sasa wananchi wanamsaka mamba huyo kwa lengo la kupata mabaki ya mwili. Rulensi ameacha mtoto wa miezi miwili.