Mwananchi yapanda mti, yazindua picha maalumu kumbukumbu ya miaka miwili ya Azory Gwanda

Muktasari:

Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, wazalishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, leo Novemba 21, 2019 imepanda mti na kuzindua picha maalumu kama ishara ya heshima na kumkumbuka mwandishi wake Azory Gwanda.


Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, wazalishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, leo Novemba 21, 2019 imepanda mti na kuzindua picha maalumu kama ishara ya heshima na kumkumbuka mwandishi wake Azory Gwanda.

Matukio hayo mawili yametokea ikiwa ni miaka miwili kamili tangu Azory, ambaye alikuwa akiandikia magazeti ya kampuni hiyo, kutoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana akiwa anaripoti habari za mauaji yaliyokuwa yakitokea Wilaya Kibiti mkoani wa Pwani.

Shughuli za kupanda mti na kuzindua picha maalumu ziliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi, Francis Nanai ambaye amesema kwamba kampuni inamkumbuka Azory kama mwandishi mahiri na jasiri ambaye alithubutu kuendelea na kazi yake hata katika mazingira ambayo yalikuwa na changamoto nyingi.

Mhariri wa jamii wa kampuni ya Mwananchi na mwandishi mkongwe Tanzania, Ndimara Tegambwage amesema kwamba kupandwa kwa mti huo kunaashiria kwamba tasnia ya habari itaendelea kustawi nchini Tanzania licha ya kuwepo kwa changamoto nyingi zinazokwamisha kazi za waandishi.

Kwa upande wake mwandishi wa habari wa Mwananchi ambaye aliongea kwa niaba ya waandishi wa habari wengine wa kampuni hiyo, Dk Tumaini Msowoya alliomba Serikali kuongeza juhudi za kutafuta mahala alipo Azory na kusisitiza kwa waandishi wengine kuzingatia weledi katika kazi zao na kuzifanya bila woga.