Mwandishi amuomba radhi kinda wa Barcelona Ansu Fati

Saturday October 24 2020
bakapic

Barcelona, Hispania (AFP). Mchezaji nyota anayechipukia katika klabu ya  Barcelona, Ansu Fati Alhamisi ameombwa radhi na moja ya magazeti makubwa Hispania, siku mbili baada ya mwandishi wa habari, Salvador Sostres kumfananisha mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 17 na “mmachinga mweusi ambaye ghafla unamuona akifukuzwa" na polisi.

Sostres alifanya ufananisho huo katika ripoti yake ya mechi iliyochapishwa na gazeti la ABC baada ya Barca kuitandika Ferencvaros ya Hungary kwa mabao 5-1 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya Jumanne.

Fati aliwapa wenyeji bao katika mechi hiyo baada ya  Lionel Messi kufunga bao la kwanza kwa njia ya penati.

Katika kuomba radhi, Sostres aliandika “nasikitishwa na kutoeleweka kwa aina yoyote” na kwamba alichotaka ni “kusifu uzuri wa uchezaji wa Ansu.”

Aliandika kuwa "Ansu akiwa kamili ana kitu kama swala, kama muuzaji bidhaa wa mitaani ambaye ghafla unamuona akikimbia pembeni ya Paseo de Gracia wakati mtu anapoanza kupiga kelele... (akisema) huyo ni polisi amewasili.”

Mshambuliaji wa Barcelona, Antoine Griezmann alikuwa miongoni mwa watu wengi waliochukizwa na ufananisho hayo.

Advertisement

Mshambuliaji huyo aliyetwaa Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa, alimtetea kinda huyo katika akaunti yake ya Twitter, akilaumu maneno ya Sostres kuwa ni ya kibaguzi.

“Ansu ni kijana asiye wa kawaida ambaye anastahili heshima kama binadamu,” Griezmannaliandika akimtetea Fati, ambaye ni raia wa Hispania na mchezaji wa timu ya taifa ambaye alizaliwa Guinea-Bissau.

Advertisement