Mwandishi wa habari Tanzania achukuliwa kwa nguvu nyumbani kwake, polisi wakana

Muktasari:

Mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera anayeandikia magazeti ya ndani na nje ya Tanzania anadaiwa kuchukuliwa kwa nguvu na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi.

Dar es Salaam. Mwandishi wa habari za uchunguzi nchini Tanzania, Erick Kabendera anadaiwa kuchukuliwa kwa nguvu na watu wanaodaiwa kuwa ni polisi nyumbani kwake nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam eneo la Mbweni.

Kabendera ambaye anaandikia magazeti ya ndani na nje ya Tanzania, inaelezwa amechukuliwa leo jioni Julai 29, 2019 na watu hao.

Mmoja wa wana ndugu ambaye ameomba hifadhi ya jina lake amesema, “Kabendera amechukuliwa na watu sita ambao walifika nyumbani kwake na kuingia kwa nguvu wakiwa na gari aina ya Toyota Alphard.”

“Watu hao walijitambulisha lakini hawakutoa vitambulisho vyao na wala hawakuficha nyuso zao na walisema wanamchukua (Kabendera) wanampeleka Polisi Oysterbay. Kabla ya kuondoka, walichukua simu ya Kabendera na ya mke wake,” amesema

Loy Kabendera ambaye ni mke wa Erick akizungumza na Mwananchi usiku huu wa leo Jumatatu amesema, watu hao walifika nyumbani na kujitambulisha kwamba ni polisi lakini hawakuwa tayari kutoa vitambulisho na wakalazimisha kuingia ndani.

Loy anasema walimchukua Erick kwa nguvu hali iliyowafanya baadhi ya majirani kufika kushuhudia tukio hilo na wale waliodiriki kupiga picha walinyang’anywa simu zao na askari  hao.

Mwananchi limewatafuta Kamanda wa Polisi Kinondoni, Dar es Salaam nchini Tanzania, Mussa Taibu pamoja na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kuhusu taarifa za Kabendera na kwa pamoja wamesema hawana taarifa ya tukio hilo huku wakiahidi kufuatilia.

 “Sina taarifa kaka, kufuatilia tutafuatilia ndiyo kazi yetu, taarifa iwe ya uongo au kweli tunafuatilia,” amesema Mambosasa wakati Kamanda Taibu akichukua majina ya mwandishi huyo (Erick Kabendera) kwa ajili ya kufuatilia zaidi kabla ya kutoa ufafanuzi hapo baadaye.

Mwaka 2012, Kabendera alitunukiwa tuzo ya mwandishi mahiri katika kipengere cha habari za Elimu kupitia Tuzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari Tanzania mwaka 2011 (EJAT).

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea