VIDEO: Mwandishi wa habari Tanzania afunguliwa kesi ya utakatishaji fedha

Mwandishi wa habari za uchunguzi Erick Kabendera akiwa chini ya ulinzi katika mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.Picha na Said Khamis

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imemfikisha mahakamani mwandishi wa habari nchini humo, Erick Kabendera na kumfungulia mashtaka matatu ikiwamo la utakatishaji fedha.

Dar es Salaam. Mwandishi wa Habari za Uchunguzi, Erick Kabendera amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam  nchini Tanzania na kusomewa mashtaka matatu ikiwamo la utakatishaji fedha.

Kabendera amefikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu Agosti 5, 2019 ambapo amesomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustino Rwezile.

Mashtaka yanayomkabili Kabendera ni kupanga na kushiriki mtandao wa uhalifu, kukwepa kodi zaidi ya Sh173 milioni na utakatishaji fedha zaidi ya Sh173 milioni.

Upande wa mashtaka umesema upelelezi bado haujakamilika hivyo Hakimu Rwezile ameiahirisha kesi hiyo hadi Agosti 19, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Kutokana na mashtaka hayo, upande wa utetezi, umeyaondoa maombi ya dhamana yaliyokuwa yameyawasilishwa mahakamani hapo kutokana na kesi iliyofunguliwa na Serikali ya Tanzania dhidi ya mwandishi huyo wa habari kutokuwa na dhamana.

Kabendera amepandishwa mahakamani ikiwa ni siku ya saba tangu alipokamatwa na Polisi wa Tanzania Julai 29 mwaka 2019 akiwa nyumbani kwake Mbweni, Dar es Salaam nchini Tanzania.

Siku iliyofuata, Julai 30, 2019, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa akizungumza na waandishi wa habari alisema walimshikilia mwandishi huyo kwa mahojiano ya uraia wake.

Mambosasa alisema walimkamata Kabendera baada ya kupelekewa wito wa kufika polisi lakini akakaidi.