VIDEO: Mwenyekiti Bavicha asema atawania urais Tanzania mwaka 2045

Muktasari:

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Mkoa wa kichama Temeke jijini Dar es Salaam, Hilda Newton ametaja ndoto yake ya kuwania urais wa Tanzania mwaka 2045.


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Mkoa wa kichama Temeke jijini Dar es Salaam, Hilda Newton ametaja ndoto yake ya kuwania urais wa Tanzania mwaka 2045.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi Tabata Dar es Salaam juzi Jumanne Oktoba 15,2019  Hilda amesema, “kwanza  ndoto yangu kubwa ni kuja kuwa Rais wa Tanzania mwaka 2045.”

Akifafanua kwa nini anasubiri hadi miaka 26 ijayo kutimiza ndoto hiyo, amesema lazima iwe hivyo kwa kuwa ili kuwania urais wa Tanzania lazima uwe umetimiza miaka 40.

Hilda ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 27 amesema, “ “ningekuwa nina umri huo (miaka 40) hata mwakani ningegombea ila kwa sasa nitagombea unaibu katibu mkuu wa Bavicha Tanzania Bara.”

Hilda ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa mkoa wa Bavicha katika uchaguzi wa ndani ya chama, amesema kuchaguliwa kwake mbali na kuwa ni uthibitisho wa uwezo wake kisiasa, umeweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuukwaa uwenyekiti wa Bavicha katika Mkoa huo.

“Ushindi huu ni baraka unaongeza nafasi ya wanawake kuaminiwa kisiasa na ni mwanzo mzuri wa safari yangu ya kuwa Rais wa Tanzania mwaka 2045,” amesema.

Katika uchaguzi huo amesema ushindani ulikuwa mkubwa kutoka kwa wagombea watatu, yeye akiwa mwanamke pekee lakini aliwashinda wote.

“Hii inanipa tafsiri kwamba sasa hivi watu wameanza kuelewa, mfumo dume unaanza kupungua na ushiriki wa wanawake kwenye siasa umeongezeka sana,” amesema

Amesema kuna vijana   hawaamini kama mwanamke anaweza kuwaongoza kwa sababu Temeke hawakuwahi kuongozwa na mwanamke tangu baraza hilo lianzishwe.

Alipoulizwa nini anawaahidi waliomchagua amesema, “kikubwa nilichowaahidi ni kuongeza idadi ya wajumbe wanawake kwa sababu ndani ya ukumbi mwanamke wa kupiga kura nilikuwa mmoja tu, niliwaambia wakati ujao watakuwa wengi.”

Kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019,  Hilda amewataka vijana kujitokeza kujiandikisha ili kushiriki uchaguzi huo, kusisitiza kufanya hivyo pia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.