Mwezi wa majonzi vifo vya kusikitisha Tanzania

Muktasari:

Mwezi Agosti umekuwa wa majonzi kutokana na vifo vya ajali ya Morogoro huku mauaji ya kusikitisha yakitokea katika baadhi ya mikoa nchini Tanzania


Dar es Salaam. Agosti mwaka huu umekuwa mwezi wa majonzi sehemu mbalimbali nchini kutokana na matukio ya mauaji na vifo kutokea. Mbali na msiba wa Taifa wa ajali ya moto iliyotokea mjini Morogoro na kusababisha vifo vya watu 100 hadi sasa yafuatayo ni baadhi ya matukio ya mauaji yaliyotokea wiki hii mwezi huu.

Agosti 18 jijini Arusha mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Arusha Meru, Faisal Salimu (19) alijiua kwa kujipiga risasi kwa kutumia bunduki ya baba yake aina ya Rifle Winchester.

Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Jonathan Shan alisema mwanafunzi huyo alijipiga risasi kwenye paji la uso na uchunguzi wa awali ulibaini alikuwa anasumbuliwa na msongo wa mawazo.

Agosti 18 hiyohiyo mkoani Geita, Efrazia Maneno (22) mkazi wa Kijiji cha Nyaseke kata ya Bulela alijinyonga hadi kufa baada ya kumnyonga mwanaye mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Dismas Kisusi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Mkoani Shinyanga, Kamanda wa Polisi, Richard Abwao alipozungumza na waandishi wa habari Agosti 18, alisema wanawashikilia watu wanne wakiwemo ndugu watatu kwa tuhuma za mauaji mama na mwanaye kwa ahadi ya malipo ya Sh2.2 milioni.

Watuhumiwa hao walitenda tukio hilo kati ya Juni 11 na Julai 18 na watuhumiwa wote wamekiri kuhusika.

Katika tukio jingine, Agosti 15, Mkazi wa kijiji cha Kinku tarafa ya Mungaa wilayani Ikungi, Editha Kanisi (49) aliuawa kwa kukatwa kwa  kisu cha kukatia majani shingoni na kichwani na mume wake Joseph Wilbroad (53).

Baada ya Joseph kufanya mauaji hayo wananchi wenye hasira kali nao walimshambulia kwa silaha na kumuua. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.