Mwili wa polisi aliyeuawa Hai waagwa

Muktasari:

Askari huyo aliuawa usiku wa  kuamkia Aprili 13,2020 na kutupwa kwenye mtaro  karibu na mgahawa wa chakula bora, mita chache kutoka kituo cha polisi cha Wilaya ya Hai.

Hai. Mamia ya wananchi wa Wilaya ya Hai, leo wamejitokeza kuaga mwili wa askari wa upelelezi kituo cha Polisi Kia, Sajenti  Juma Chriphord Yango (59),  aliyeuwawa na watu wasiojulikana na mwili wake kutupwa kwenye Mtaro.

Askari huyo aliuwawa usiku wa  kuamkia Aprili 13,2020 na kutupwa kwenye mtaro  karibu na mgahawa wa chakula bora, mita chache kutoka kituo cha polisi cha wilaya ya Hai.

Vilio vilitawala msiba huo huku  wanafamilia wakisikika wakisema; “amewakosea nini kwa nini mumuue kikatili hivyo.”

Akizungumza  leo  Jumatano Aprili 15, 2020 kwenye Ibada ya kuuaga mwili wa aAskari huyo iliyofanyika nyumbani kwake, Mchungaji wa Kanisa la  Waadventista  Sabato Hai, William Sinyaw ameasa watu waishi kwa upendo na amani kwa kuwa hakuna anayejua  siku yake ya mwisho hapa duniani.

Aidha, aliwataka waumini kuliishi neno la Mungu linaloweza kusaidia kuepuka magonjwa ya hatari yanayotokana na matendo ya wanadamu yamchukizayo Mungu.

“Kwa sasa dunia inapambana na virusi hatari vya corona, lakini bado watu wanafanya ukatili mwingine wa kuendelea kumchukiza Mungu. Huyu askari ameuawa ameacha mjane na watoto watatu na mjukuu mmoja, halafu wanadamu kwa makusudi wanaamua kuatisha uhai wake, hii ni dhambi,” alisema Sinyaw.

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Mkuu wa kituo cha Polisi  Wilaya ya Hai, Lwelwe Mpina amewataka wananchi kutoa taarifa  zitakazolisaidia Jeshi la Polisi kuwapata waliofanya ukatili huo.

Maiti ya Yango imekutwa na jeraha kisogoni linaloonyesha kuwa alipigwa na kitu chenye ncha kali.