Mwili wa rubani mwanafunzi ndege iliyoanguka wachukuliwa Serengeti

Muktasari:

  • Ndege ya Kampuni ya Auric imekwenda kuuchukua mwili wa rubani mwanafunzi uliokuwa umehifadhiwa katika zahanati ya Soronera ndani ya Hifadhi ya Serengeti nchini Tanzania na kuupeleka mkoani Arusha nchini humo kwa mazishi.

Serengeti. Mwili wa rubani mwanafunzi Nelson Urutu umechukuliwa na ndege ya Kampuni ya Auric Air na kuupeleka mkoani Arusha nchini Tanzania kwa taratibu za mazishi.

Orutu amefikwa na mauti leo Jumatatu asubuhi Septemba 23,2019 akiwa na rubani wa ndege ya kampuni hiyo yenye namba 5H-AAM, Nelson Mabeyo iliyoanguka katika uwanja mdogo wa ndege ya Soronera ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Ndege hiyo imeondoka katika uwanja huo wa Soronera saa 10 jioni kwenda Arusha.

Taratibu za usafirishaji wa mwili zilizohusisha wafanyakazi wa kampuni hiyo, uongozi wa hifadhi chini ya Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Massana Mwishawa amesema tukio hilo limewashtua sana kwa kuwa ni mara ya kwanza kutokea na kuua watu.

Kamishina wa Uhifadhi Kanda ya Magharibi, Martin Loiboki ameomba taratibu za uchunguzi zifanyike kwa wakati.

Mapema mwili wa rubani wa ndege hiyo Nelson Mabeyo ambaye ni mtoto wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Tanzania, Venance Mabeyo umechukuliwa kupelekwa Dar es Salaam kwa Helikopta ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).