MAKALA ZA MALOTO: Mzee Malecela ana deni kubwa kuandika kitabu

Hivi karibuni nilitazama simulizi ya maisha ya aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza, John Malecela.

Nasema hivyo kwa sababu kuna eneo alilisimulia katika mahojiano yake na moja ya vyombo vya habari hapa nchini, likanifanya nione ni kwa kiasi gani veterani huyo wa siasa alivyo na deni kubwa la kulipa kwa Taifa.

Alikuwa akisimulia jinsi uhusiano wa Tanzania na Uganda ya Idi Amin ulivyoanza kuharibika na yeye alivyocheza eneo lake kama Waziri wa Mambo ya Nje kujaribu kupata suluhu. Malecela alisimulia mkasa wa mwaka 1974 kuwa wanafunzi wa Kitanzania waliokuwa wanasoma Uganda, Chuo Kikuu cha Makerere na Chuo cha Mafunzo ya Urubani cha Soroti, waliwekwa kizuizini na kukawepo tishio la kuuawa. Kutokana na tishio hilo, aliyekuwa Rais, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alimtuma kwenda kufanya mazungumzo na Amin ili kumuomba awaache wanafunzi waliokuwa wanashikiliwa.

Kwa mujibu wa Malecela, uamuzi wa kwenda Uganda kuonana na Amin ulitaka ujasiri na aliweka rehani maisha yake. Amin alikuwa mtu ambaye angeweza kufanya lolote na wakati wowote bila kujali wala kuhofia chochote.

Malecela alikwenda Uganda na alionana na Amin. Mazungumzo ya kwanza alimweleza Malecela kuwa Tanzania chini ya Mwalimu Nyerere, ilikuwa inapingana na utawala wake. Lakini Malecela alimjibu kuwa Serikali ya Tanzania haikuwa na tatizo naye kabisa.

Kwa jibu hilo, Amin aliagiza apelekewe gari ili amwendeshe Malecela mitaa mbalimbali ya Kampala.

Gari alilopelekewa Amin alipoliwasha halikuwaka, ikabidi lipelekwe lingine haraka. Amin aliendesha, Malecela aliketi upande wa abiria. Wawili tu. Hawakuwa na ulinzi anasema alitaka amwonyeshe Malecela jinsi anavyopendwa Uganda.

Walipofika sokoni Nakasero Kampala, Amin aliegesha gari na watu walipomwona walianza kumshangilia. Amin akamtambulisha Malecela kisha akasema: “Mmeona? Mimi sina tatizo na Nyerere wala Tanzania. Huyu hapa ni Waziri wa Nyerere, amekuja kututembelea. Na mimi nimemleta mumuone muone sina tatizo na Nyerere. “Kuanzia leo nisisikie Mtanzania yeyote anasumbuliwa hapa Uganda. Sisi na Watanzania ni ndugu.” Walipotoka sokoni walizunguka maeneo mengine ambayo Amin aliendelea kumtambulisha Malecela na kusisitiza undugu wa Tanzania na Uganda. Wakati Malecela akifanya mazungumzo na Amin, upande wa pili kulikuwa na operesheni ya kuwatorosha wanafunzi waliokuwa wanasoma Makerere na Soroti. Wale wa Makerere wote walirejeshwa Tanzania salama. Shida ilikuwa kwa wale wa Soroti, wao walisema wasingeondoka kwa sababu walibakiza muda mchache ili kufanya mitihani yao ya mwisho ya kumaliza masomo ya urubani. Soroti ni chuo kilichoanzishwa na Serikali za Tanzania, Uganda na Kenya chini ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jumla ya wanafunzi wa Tanzania waliokuwa wanasoma Soroti ni 21. Malecela aliporejea Tanzania na baada ya kubainika wanafunzi wa Kitanzania waliokuwa Makerere tayari walishatoroshwa, wale 21 wa Soroti wote waliuawa na askari wa Amin.

Upo uhusika wa Amin ambao huchezwa kwenye filamu mbalimbali. Wengi hudhani Amin anasingiziwa au uhusika wake wa kwenye filamu huongezewa chumvi. Hata hivyo, ukimsikiliza Malecela, unabaini kwamba kumbe hasingiziwi. Taratibu historia inafutika, uongo pia unasemwa. Wapo Watanzania huingia mkumbo wa kusema vita ya Kagera, uchokozi ulianzishwa na Tanzania. Simulizi ya Malecela jinsi wanafunzi wa Soroti walivyouawa, vilevile wa Makerere walivyotoroshwa, inaonyesha ni kwa kiasi gani Tanzania ilivumilia uchokozi wa Amin kwa muda mrefu.

Wanafunzi 21 wa Soroti pengine wangekuwa marubani wa kwanza wa Tanzania, maana walikuwa hatua ya mwisho kabisa ya masomo yao. Kuuawa kwao ilikuwa hasara kubwa kwa nchi na familia zao. Vita ya Kagera ilianza rasmi Novemba 1978 baada ya majeshi ya Uganda kuvamia mkoa wa Kagera. Ilikuwa miaka minne baada ya marubani watarajiwa 21 wa Tanzania kuuawa. Malecela alilisimulia kuhusu Tanzania ilivyowawezesha Wakenya kuushinda Ukoloni. Wakati huo Malecela akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, alishuhudia magari ya Serikali yakibadilishwa namba za usajili ili yakatumike Kenya kwenye harakati za kupigania uhuru. Ni simulizi yenye ukweli kuwa Tanzania chini ya uongozi wa Nyerere, ilikuwa daraja la uhuru wa nchi nyingi Afrika. Simulizi hizo zinaonyesha ni kiasi gani Malecela ana deni la kulipa kwa Taifa kwa kuandika kitabu.

Malecela anapaswa kuandika kitabu ambacho kitafanya simulizi aliyotoa kwa ufupi, isomwe vizazi na vizazi kwa urefu na usahihi.

Hakuna nchi ya Afrika iliyopata uhuru baada ya Tanganyika ambayo ilifanikisha vuguvugu lake pasipo ushiriki wa Tanganyika na baadaye Tanzania.

Upotoshaji kuhusu vita ya Kagera, utadhibitiwa ikiwa tu viongozi maveterani wenye historia ya nchi kichwani, wataamua kuweka waliyonayo kichwani kwenye maandishi.

Malecela atambue kuwa historia itamheshimu mno kama ataandika kitabu cha maisha yake ya kisiasa na historia ya nchi kidiplomasia.