Mzee wa Upako atoa neno serikali za mitaa

Muktasari:

  • Mchungaji Lusekelo ametaka wananchi wapewe uhuru wa kuchagua viongozi wanaowataka kutoka vyama vya upinzani katika uchaguzi wa serikali za mitaa 

Wakati mjadala mkubwa nchini Tanzania ukiendelea kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa baada ya baadhi ya vyama kadhaa vya upinzani kutangaza kususia uchaguzi huo kwa madai ya kuonewa kwa wagombea wao, wadau mbalimbali wametoa maoni yao kuhusu uchaguzi huo.

Moja ya watu waliotoa maoni yao ni Mchungaji wa Kanisa la GRC, Jijini Dar es Salaam, Antony Lusekelo (Mzee wa Upako) ambaye anasema wananchi wanatakiwa kupewa uhuru wa kuchagua viongozi wanaowataka kutoka kwenye vyama vya upinzani.

“Vyama vya siasa visiingiliwe, vishindane na vikubaliane na matokeo baada ya uchaguzi.

“Sisi tunaendelea kuwapatia watu elimu kwamba wawachague viongozi wasioendekeza rushwa na watakaofaa kuongoza kwenye maeneo yao,” alisema Lusekelo.

Vyama vya upinzani vikiwemo Chadema na ACT- Wazalendo wametangaza kujitoa katika uchaguzi huo baada ya kudai kuwa wagombea wao wengi wameondolewa katika uchaguzi huo kinyume na taratibu .