SHERIA: Mzungu wa unga aongezewa adhabu

Muktasari:

  • Mfungwa huyo alikuwa akipinga adhabu aliyopewa awali na Mahakama Kuu

Moshi. Mkazi wa Mwembechai jijini Dar es Salaam, Sophia Kingazi aliyefungwa miaka 20 na kulipa faini ya Sh10 milioni kwa kusafirisha dawa za kulevya, ameongezewa adhabu na Mahakama ya Rufaa.

Kutokana na kuongezewa adhabu hiyo, mwanamke huyo sasa atalipa faini ya Sh506 milioni ambayo ni mara tatu ya thamani ya dawa za kulevya alizokamatwa nazo badala ya Sh10 milioni.

Sophia alihukumiwa adhabu hiyo Juni 15, 2016 na Jaji Benedict Mingwa wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Cocaine zenye thamani ya Sh168.9 milioni.

Wakati mabegi yake yakipitishwa katika mashine ya ukaguzi uwanja wa Kia, maofisa usalama walibaini kuna vitu visivyoeleweka na ukaguzi zaidi ukabaini kuna gramu 3379.54 za Cocaine.

Upande wa mashtaka uliita mashahidi 11 ambao waliitbitishia Mahakama mshtakiwa kutenda kosa hilo licha ya kulikana begi lililokuwa na dawa hizo lililokuwa limewekwa alama (label) ya S. Kingazi.

Jaji Mingwa alimhukumu kutumikia kifungo cha miaka 20 jela na kulipa faini ya Sh10 milioni, lakini hakuridhika na hukumu hiyo na kukata rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania iliyoketi Arusha.

Miongoni mwa sababu zake nne za rufaa yake, alidai jaji alikosea kisheria kwa kumtia hatiani kwa kosa ambalo halikuthibitishwa na pia alikosea kutozingatia kuwa mnyororo wa utunzaji vidhibiti ulikatika.

Hata hivyo, katika hukumu yao, jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo; Shaaban Lila, Mwanaisha Kwariko na Lugano Mwandambo walizikataa sababu za rufaa na kubariki kifungo cha miaka 20.

Kuhusu kiwango cha faini, majaji hao walikubaliana na hoja za mawakili wa Serikali kwamba kiwango cha faini kilipaswa kuwa mara tatu ya thamani ya dawa hizo, hivyo kuamru alipe na faini ya Sh506.9 milioni.