NBS yazungumzia mfumuko wa bei

Mkurugenzi wa takwimu za sensa na kijamii, Ruth Davison

Muktasari:

  • Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetangaza kupungua kwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka unaoishia Agosti 2019 hadi asilimia 3.6 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka unaoishia Julai 2019.

Dodoma. Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetangaza kupungua kwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka unaoishia Agosti 2019 hadi asilimia 3.6 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka unaoishia Julai 2019.

Akizungumza jana Septemba 9,  2019 kaimu mkurugenzi wa takwimu za sensa na kijamii, Ruth Davison amesema hiyo inamaanisha kasi ya mabadiliko ya bidhaa na bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Agosti,  2019 imepungua ikilinganisha na kasi iliyokuwepo kwa mwaka unaoishia Julai, 2019.

"Farisi za bei zimeongezeka hadi 116.06 mwezi Agosti 2019 kutoka 112.01 mwezi Agosti 2018," amesema.

Amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Agosti 2019  kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia Agosti 2019 zikilinganishwa na bei za Agosti  2018.

Amesema baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizopungua bei kwa Agosti 2019 zikilinganishwa na bei za Agosti 2018 ni mafuta ya taa kwa asilimia 2.6 na petroli kwa asilimia 4.3.

Nyingine ni  majiko ya gesi kwa asilimia 1.4, gharama za kufanya ukarabati nyumba kwa asilimia 1.7 na bidhaa za usafi binafsi kama mafuta ya nywele kwa asilimia 1.3.