NEC yabaini Watanzania wengi wamepoteza kitambulisho cha mpiga kura

Muktasari:

  • Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) imebaini Watanzania wengi wamepoteza kitambulisho cha mpiga kura.

Dodoma. Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) imebaini Watanzania wengi wamepoteza kitambulisho cha mpiga kura.

Hayo yamebainika wakati wananchi wakijiandikisha kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Akizungumza leo Jumatano Oktoba 16, 2019 katika mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi mjini Dodoma mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage amesema

" Tume inapenda kuchukua fursa hii kuwasisitiza na kuwakumbusha wapiga kura kutunza kadi zao na wale waliopoteza kadi kuhakikisha wanakumbuka taarifa kwa usahihi ili waweze kuhudumiwa kwa haraka watakapokuwa vituoni.”

Ametaja changamoto nyingine ni wapiga kura kutokuwa na uhakika wa kukumbuka majina yao wanapofika kurekebisha taarifa zao na hivyo kuchukua muda mrefu kituoni kutafuta majina yao kwa usahihi.

Hata hivyo, Jaji Kaijage amesema uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Wapigakura katika kata ya Kihonda mkoani Morogoro na Kibuta mkoani Pwani umeonyesha mafanikio baada ya  watu wengi kujitokeza kujiandikisha.

Amesema shughuli ya kuhakiki vituo kwa upande wa Dodoma liliongeza vituo vya kuandikisha wapiga kura kutoka  2,606 vilivyokuwepo mwaka 2015 hadi vituo 2,686.

Amesema kuna vituo 80 vya kuandikisha wapiga kura katika mkoa wa Dodoma.

Shughuli za uboreshaji katika awamu ya kwanza zimekamilika mikoa 10 ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Simiyu, Mara, Mwanza, Geita, Shinyanga, Kagera na Kigoma.

Shughuli hiyo inaendelea hivi sasa  katika mikoa ya Tabora, Katavi na Rukwa.