NEC yatoa ratiba uboreshaji daftari wapiga kura Dar, Pwani

Muktasari:

Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka 2020 ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini humo imekwisha kuanza uboreshaji wa daftari hilo kwa kutumia teknolojia  ya  kielektroniki ya biometriki (BVR).
Teknolojia hii huchukua taarifa za mtu za kibaiolojia na kuzihifadhi katika Kanzidata (Database) kwa ajili ya utambuzi na ndio teknolojia iliyotumika kuandikisha wapiga kura mwaka 2015.

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania imesema uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia teknolojia  ya  kielektroniki ya biometriki (BVR) katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani itaanza Ijumaa Februari 14 hadi 20, 2020.

NEC imesema vituo  vitafunguliwa kuanzia saa 2 asubuhi na kufungwa saa 12 jioni huku ikiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kuwa na haki ya kuchagua viongozi wanaowataka katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka 2020 ukihusisha madiwani, wabunge na Rais.

Hivi karibuni  Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage akizungumza na wadau wa siasa jijini Dar es Salaam alisema uboreshaji wa daftari hilo umefanyika katika mikoa yote ya Tanzania isipokuwa Dar es Salaam na Pwani.

Jaji Kaijage alisema kwa mujibu wa Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 21(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292, Tume inapaswa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya uchaguzi mkuu mmoja na uchaguzi mkuu mwingine unaofuatia.

Alisema ni matarajio yao baada ya kukamilisha uboreshaji huu wa awamu ya kwanza watakutana tena na wadau kuwafahamisha kuhusu uboreshaji wa awamu ya pili ambao kwa sasa maandalizi yake yanaendelea.

Jaji Kaijage alisema kabla ya kuanza uandikishaji, uhakiki wa vituo vya kuandikisha Wapiga Kura nchi nzima ulifanyika mwaka  2018. Lengo lake lilikuwa ni kuona kama vituo hivyo bado vipo na kama bado vina sifa na hadhi ya kuwa vituo vya kuandikisha wapiga kura, kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Uchaguzi.

Alisema uhakiki huo ulilenga kuangalia iwapo kuna maeneo yanayohitaji kuongeza Vituo.

Kutokana na uhakiki huo, vituo vya kuandikisha wapiga kura kwa nchi nzima viliongezeka kutoka vituo 36,549  hadi 37,407.  Kwa Mkoa wa  Dar es Salaam  Vituo hivyo viliongezeka  kutoka 1,614 vya kuandikishia wapiga kura vilivyokuwapo mwaka 2015,  hadi kufika vituo 1,661 mwaka 2020.

“Ni vituo 47 tu vya uandikishaji wapiga kura vilivyoongezeka katika Mkoa huu wa Dar es Salaam,” alisema Jaji Kaijage