NGUVU YA WANANCHI: Rais Magufuli aonya CCM kuanguka

Mwanza. Mara kadhaa baadhi ya viongozi na makada wa CCM wamekaririwa wakitamba kuwa chama hicho kitaendelea kuongoza kwa miaka mingi ijayo kwa kuwa hakuna upinzani makini, lakini jana Rais John Magufuli ameonya dhidi ya kubweteka huko.

Anaona CCM inaweza kuanguka kama vyama vingine vilivyopigania ukombozi barani Afrika na baadaye vikajisahau.

CCM ni moja ya vyama vichache vikongwe vilivyopigania uhuru ambavyo bado viko madarakani licha ya mabadiliko tofauti ya kisiasa barani Afrika yaliyosababisha baadhi kuondolewa madarakani katika boksi la kura.

Jana, Rais alionya dhidi ya kubweteka huko, akisema CCM inaweza kupoteza dola iwapo viongozi wake watajisahahu na kuanza kuongoza kwa mazoea bila kukidhi mahitaji na matarajio ya wananchi.

Alikuwa akifungua mkutano wa majadiliano ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM jijini Mwanza jana.

Alisema hata baadhi ya vyama vya ukombozi vilivyopoteza uongozi katika nchi kadhaa za Afrika viliponzwa na tabia ya kujisahahu na kuongoza kwa mazoea.

Miongoni mwa vyama vya ukombozi vilivyoondolewa madarakani na wananchi kupitia sanduku la kura ni pamoja na Kanu ya nchini Kenya, UNIPI cha Zambia, Malawi Congress Party (MCP) cha Malawi kilichoondolewa madarakani mwaka 1993.

Chama cha African National Congress (ANC) cha nchini Afrika Kusini kimeendelea kuongoza huku kikikabiliwa na ushindani mkali kutoka vyama vya upinzani ambavyo baadhi vimeundwa na waliokuwa makada wake.

“Siku mbili zilizopita, tumesheherekea maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika. Katika miaka hii yote, Chama cha Mapinduzi ndicho kinaongoza, ukiacha miaka michache ya uongozi wa vyama – Mama vya Tanu na ASP,” alisema Rais.

Tanu iliongoza harakati za ukombozi wa Tanganyika na ASP iliongoza mapinduzi ya Zanzibar. Vyama hivyo viliungana mwaka 1977 na kuunda CCM.

“Kimsingi, tangu tumepata uhuru CCM imeendelea kushika hatamu za uongozi kwa kipindi chote hiki, jambo ambalo ni nadra katika nchi nyingi za Afrika,” alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa.

“Kwa hakika, hili ni jambo la kujivunia na kujipongeza sisi wote.”

Rais alionya kuwa licha ya kila mmoja kutamani chama hicho kiendelee kushika hatamu ya uongozi kwa miaka mingine ijayo, matamanio hayo yanaweza yasifanikiwe iwapo viongozi wake watajisahau kwa kuongoza kwa mazoea na kutokidhi mahitaji na matamanio ya Watanzania.

“Ili tuweze kufahamu kama tunakidhi matarajio ya wananchi, hatuna budi kujenga utamaduni na uwezo wa kujitathimini, kujisahihisha na kubadilika. Tuepuke uongozi wa mazoea,” alisema.

“Vyama vingi vinavyojisahau na kuongoza Serikali kwa mazoea, hufikia hatua ya kupoteza imani ya wananchi na uhalali wa kisiasa. Ndicho kilichotokea kwa baadhi ya vyama vingi vilivyopigania uhuru barani Afrika. Ndugu zangu tusifikie huko.”

Mwenyekiti huyo wa CCM aliwataka wajumbe kutumia mkutano huo kutathmini utendaji wa chama na Serikali, kwa lengo la kujenga uelewa kuhusu kilikotoka, kilipo na mwelekeo wake hasa masuala mapana ya mwelekeo wa sera kwa miaka 10 pamoja na mipango mahsusi itakayotekelezwa kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025.

Mwaka 2015 CCM ilijikuta katika kipindi kigumu wakati vyama vya upinzani vilipounganisha nguvu katika uchaguzi mkuu. Magufuli alishinda kwa kura milioni 8.8--sawa na asilimia 58-- huku Edward Lowassa aliyegombea kwa tiketi ya Chadema na vyama vingine vitatu, akipata kura milioni 6.07-- sawa na takriban asilimia 39, tofauti ambayo ni ndogo kuwahi kutokea tangu kurejeshwa kwa vyama vingi mwaka 1992.

Kuimarisha CCM

Rais pia alizungumzia hatua alizochukua tangu akabidhiwe chama hicho, akisema alifanya hivyo kwa nia ya kuhakikisha CCM inakuwa imara kimuundo, kiutendaji na kiuchumi.

“Mageuzi hayo yalikuwa hayaepukiki ili kulinda uhai wa chama, kurejesha imani ya wananchi na heshima ya chama chetu. Yalijengwa kwenye dhana ya chama imara, Serikali Imara,” alisema.

“Na kusema kweli, ilikuwa ni vigumu kuzungumzia mageuzi makubwa ndani ya Serikali, ilihali chama kilichokabidhiwa dola kipo hoi bin taaban. Hii ingesababisha mtanziko mkubwa wa kiuongozi.”

Alitaja baadhi ya mageuzi ya kimuundo na kiutendaji kuwa ni pamoja na kupunguza idadi ya wajumbe wa NEC kutoka 342 hadi 168, kuwaondoa makatibu wa mikoa katika orodha ya NEC, kuondoa kada za Katibu msaidizi na Mhasibu wa wilaya na mkoa na kuunganisha utumishi wa chama na jumuiya zake chini ya usimamizi wa sekretarieti ya halmashauri Kuu.

“Kiuchumi, tulibaini kwamba, pamoja na uwingi wa rasilimali, mapato ya chama yalikuwa ni kidogo na kilikuwa hakiwezi kujiendesha kwa sehemu kubwa mali na rasilimali za chama zilikuwa zikiwanufaisha watu binafsi, hususan viongozi wachache waliokuwa wamejimilikisha mali na rasilimali hizo,” alisema.

Alitaja baadhi ya mali zilizorejeshwa mikononi mwa CCM kutoka kwa watu binafsi kuwa ni pamoja na kituo cha runinga cha Channel Ten, majengo, viwanja, vitalu vya madini na vituo vya mafuta.

Alisema jitihada hizo pamoja na matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa usimamizi na uendeshaji wa mali na rasilimali za CCM, zimeongeza mapato ya chama kutoka Sh46.1 bilioni mwaka 2015/16 hadi kufikia Sh59.8 bilioni 2018/19, sawa na ongezeko la asilimia 30.

Rais alisema tathmini mpya ya mali za chama iliyofanyika katika mikoa 13 pekee, imepandisha thamani za mali za chama hicho kutoka Sh41.033 bilioni mwaka 2016/17 hadi Sh974.9 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 2275.3.

“Jambo jingine la kujivunia na kufurahisha zaidi ni kwamba katika miaka minne iliyopita, chama chetu kimeendelea kupokea wanachama kutoka vyama vya upinzani, wakiwemo wabunge na madiwani. Hii imepelekea ruzuku ya chama kuongezeka kutoka Sh12.4 bilioni mwaka 2015/16 hadi Sh13.5 bilioni kwa mwaka hivi sasa,” alisema huku wajumbe wakipiga makofi.

Rais pia alizungumzia hujuma alizosema zinafanywa na watu wasioitakia mema Serikali.

“Watu hao kamwe hawataki kuona tunadhibiti rasilimali zetu ambazo walikuwa wanazivuna na kuzisafirisha wanavyotaka bila kuulizwa na mtu,” alisema.

Alisema baadhi ya miradi mikubwa inayoharakisha maendeleo ambayo watu hao wasingependa kuona inaendelea kuwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme Nyerere katika bonde la mto Rufiji, elimu bila malipo na umeme vijijini.

“Wakati mwingine watatumia asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali kujifanya wanatufundisha demokrasia na haki za binadamu wakati wao wanavunja misingi hiyo kwa kujenga mifumo ya kinyonyaji kwa kuchochea machafuko na kuingilia uhuru wa Mataifa mengine,” alisema.

Wakati akitangaza mpango wa Tanzania wa kuhakikisha idadi ya watalii wanaotembelea nchini inaongezeka kutoka 1.5 milioni ya sasa hadi kufikia 10 milioni miaka kumi ijayo, Rais Magufuli ameagiza majeshi ya ulinzi na usalama kuanzisha na kutekeleza miradi ya uzalishaji mali.

Rais amesema hayo wakati ukiendelea mjadala kuhusu nia ya Tanzania kujitoa Mahakama ya Afrika kutokana na chombo hicho kukiuka taratibu kuhusu vifungu ambavyo vinaruhusu taasisi za kijamii na watu binafsi kuishtaki Serikali kwa kukiuka haki za binadamu, baadhi ya taasisi zikipinga vikali uamuzi huo na kutaka Serikali itafute ridhaa ya wananchi kwanza.

Mawasiliano, umeme

Katika sekta ya mawasilino Rais Magufuli alisifu mafanikio ya kampuni ya simu ya TTCL akieleza kuwa ni lengo la Serikali kuona shirika hilo la umma linamiliki asilimia 50 ya kampuni za mawasiliano.

Kuhusu nishati ya umeme, kiongozi huyo alisema Serikali inakusudia kuongeza uwekezaji na uzalishaji wa nishati hiyo kuwezesha bei yake kushuka kufanikisha utekelezaji wa sera ya uchumi wa kati.