Naibu Waziri Kijaji atoa maagizo kwa nchi za Comesa

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa fedha na mipango aziagiza nchi wanachama wa Comesa kuondoa changamoto zinazojitokeza katika usafirishaji mizigo bandarini.

Arusha. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashantu Kijaji ameziagiza nchi  wanachama wa  Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Mashariki na Kusini  mwa Afrika (Comesa) kuondoa changamoto mbalimbali zinazojitokeza  wakati wa usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini kwenda nchi zisizo na bandari.

Ameyasema hayo leo Jumanne Oktoba 15, 2019 jijini Arusha wakati akizungumza katika mkutano wa mwaka wa 13 wa baraza la mashirika ya bima na mamlaka za mapato kwa nchi wanachama wa Comesa uliolenga kujadili changamoto ya usafirishaji mizigo mbalimbali bandarini pamoja na kuzipatia ufumbuzi.

Dk Kijaji ameziagiza  mamlaka hizo za mapato na bima kuhakikisha mizigo yote inayoenda nchi za DRC Congo na nchi zisizo na bandari zinafika kwa wafanyabiashara walioagiza mizigo kwa wakati jambo  litakalopunguza gharama pamoja na bei kwa mnunuzi wa mwisho.

Amesema kumekuwepo na changamoto mbalimbali wakati wa usafirishaji wa mizigo hiyo ikiwemo ucheleweshaji mbalimbali pamoja na kushushwa kwa mizigo na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kwa lengo la kujipatia kipato na hatimaye kumpatia hasara kubwa mwigizaji wa mizigo hiyo.

"Nchi hizi za Comesa walikubaliana kuanzisha umoja huo wa ushirikiano wa wakurugenzi wa mashirika ya bima na mapato katika nchi hizo kwa ajili ya kudhibiti udanganyifu wa baadhi ya wafanyabiashara wasafirishaji wanaoshusha mizigo njiani kabla ya kufikisha kwenye nchi husika isiyo na bandari.”

“Hivyo uwepo wa umoja huo utaweza kuondoa changamoto mbalimbali katika nchi hizo na hivyo kuwezesha mizigo yote kufika salama bila vikwazo vyovyote," alisema

Aidha amezitaka nchi zote zilizo kwenye umoja wa jumuiya hiyo na ambazo hazipo kuhakikisha mamlaka zao za mapato na bima zinakuwa wanachama kwenye baraza hilo ili kudhibiti huo udanganyifu na kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza mapato .

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la bima la Taifa (NHC), Dk Elirehema Doriye amesema matarajio ya mkutano huo ni kuhakikisha shughuli zote za usafirishaji zinafanyika kwa wakati bila kuwepo kwa vikwazo vyovyote.

Amesema kumekuwepo na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza ikiwemo ucheleweshaji wa mizigo bandarini ambapo wamekuwa wakishirikiana na mamlaka husika za ulinzi na usalama kuhakikisha mizigo hiyo inatoka kwa wakati na kufika sehemu husika.