Naibu Waziri Manyanya amfukuza eneo la kazi bosi wa TBS Namanga

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Stella Manyanya

Muktasari:

Naibu Waziri wa viwanda na biashara aagiza kuhamishwa kituo cha kazi aliyekuwa Kaimu msimamizi wa TBS Namanga mkoani Arusha

Arusha. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Stella Manyanya amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwanda nchini humo (TBS) kumwamisha kituo cha kazi aliyekuwa kaimu msimamizi wa TBS kituo cha Namanga, Martha Suda  kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake katika utendaji kazi.

Ameyasema hayo leo Ijumaa Novemba 15, 2019 wakati akizungumza katika kituo cha ofisi hiyo kilichopo Namanga wakati alipofanya ziara yake ya kikazi.

Amesema amewahi kutoa maagizo katika kituo hicho kuhakikisha kuwa wanaorodhesha  majina ya wafanyakazi wao katika ubao wa matangazo  ili kuwarahisishia wananchi kuweza kuwapata kwa urahisi zaidi.

"Nilitoa maagizo hayo muda mrefu lakini leo nimekuja hapa nashangaa hayo maagizo hayajatekelezwa na sijui kwa nini, sasa Serikali hii haina mchezo na haipo tayari kukaa na kufanya kazi na watu wazembe kama hawa.”

“Tunaomba huyu Martha ahamishwe kituo kingine cha kazi haraka iwezekanavyo na nitafuatilia hilo," amesema Injinia Manyanya.

Manyanya amesema kwa sasa hivi nafasi hiyo itashikiliwa na Peter Musiba ambapo alimtaka kufuata sheria na kanuni huku akiwataka kuondokana na uzembe ambao umekuwa ukifanyika kituoni hapo.

Aidha alitumia nafasi hiyo kuwaagiza wakuu wote wa vituo katika mpaka huo kuhakikisha wanaorodhesha majina ya wafanyakazi wao kwenye ubao wa matangazo ili kuwarahisishia wananchi hao kuwapata kwa urahisi wafanyakazi hao  na kuondoa urasimu wa kuchelewa kupata huduma hizo.

Naye  Mkuu  wa wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe amesema kumekuwepo kwa utendaji mzuri wa kazi katika idara mbalimbali zilizopo mpakani ila kumekuwepo na malalamiko mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa na wafanyabiashara wadogo na wakubwa kuhusu kutoridhishwa na utendaji kazi wao.

Amesema malalamiko hayo yamekuwa yakichangiwa na shirika hilo kutokana na kutowapelekea taarifa  wateja popote walipo kuhusiana na utoaji wao wa huduma na namna ya kufuata sheria na taratibu za shirika hilo ili kuwarahisishia kupata huduma hizo kwa haraka bila kuwepo kwa usumbufu wowote.

"Nyie ndio mnatakiwa muwafuate hao wateja  katika maeneo  yao na kuwapa taarifa namna ya utendaji kazi wenu na sio nyie kukaa na kusubiri hadi wawafuate ofisini jambo ambalo linaibua changamoto mbalimbali pamoja na malalamiko kutokana na wengi wao kutokuwa na uelewa wa kutosha na sheria za kufuata," alisema Mwaisumbe.