Naibu waziri Kandege atoa mwanga watumiaji mabasi yaendayo haraka Dar

Muktasari:

Mwaka huu huenda Serikali ikatimiza kiu ya muda mrefu ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanaotumia mabasi yaendayo haraka baada ya Naibu Waziri wa Tamisemi, Josephat Kandege kusema kuwa  kabla ya mwaka huu kuisha, mtoa huduma mpya atakuwa amepatikana.


Dar es Salaam. Serikali imesema hivi karibuni itatangaza tenda kwa ajili ya kumpata mwendeshaji wa mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya kwanza baada ya kuisha kwa kipindi cha mpito.

Suala la upatikanaji wa mwendeshaji huyo limekuwa likitajwa kila mara na sasa Serikali kuwa ipo kwenye mchakato.

“Hapo awali tulifikia hatua nzuri lakini kutokana na mambo kadhaa, mchakato ukakwama na tukaanza upya, sasa tumefikia hatua nzuri punde tutagawa tenda na nyaraka za tenda na pengine kabla ya mwaka huu kuisha, tutakuwa tumempata mwingine,” amesema Naibu Waziri wa Tamisemi Josephat Kandege leo Jumatano Oktoba 2, 2019.

Kandege ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano wa wadau wa usafiri wa umma katika majiji ya Afrika Mashariki, anasema tatizo lililopo sio la upande mmoja bali linahusisha wadau wote wenye mradi, waendeshaji na watoa fedha ambao ni Benki ya Dunia (WB) na watoa fedha hawataki upande hata mmoja ulalamike na yakitokea manung’uniko wanasitisha.

“Watoa fedha wanataka mradi uwe kama ulivyopangiliwa awali, hawataki mwendeshaji awe ndiyo mkusanya nauli na hapo katikati kulikuwa na mambo ya kesi ndiyo maana mchakato ukasitishwa,” amesema Kandege.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Serikali  wa mabasi yaendayo haraka (Dart), Ronald Lwakatare amesema katika awamu ya pili ya mradi huo Serikali imejipanga kumpata mtoa huduma na mkusanya nauli mapema ili kuepusha usumbufu kama unaojitokeza sasa.

“Kipindi cha majaribio katika awamu hii ya kwanza tumejifunza mengi sasa tunahakikisha tunawapata washirika muhimu katika mradi, mwaka mmoja kabla ya kuanza rasmi kwa mradi huo,” amesema Lwakatare.