Nandy azikumbuka tuzo za Kilimanjaro akiwasili kutoka Marekani

Muktasari:

Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Faustina Charles maarufu Nandy amesema tuzo za Kili Music Awards (KTMA) ziliwafanya wasanii nchini Tanzania kushindana zaidi, si kusubiri kunyakua tuzo za kimataifa.

Dar es Salaam. Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Faustina Charles maarufu Nandy amesema tuzo za Kili Music Awards (KTMA) ziliwafanya wasanii nchini Tanzania kushindana zaidi, si kusubiri kunyakua tuzo za kimataifa.

Nandy anayetamba na wimbo wa ‘kiza kinene’ ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Oktoba 31, 2019 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akitokea nchini Marekani alikoshinda tuzo za Entertainment Award USA (AEAUSA) mwaka 2019.

Tuzo hizo zilitolewa wiki moja iliyopita mjini New York, Marekani huku Nandy akinyakua  kipengele cha msanii bora wa kike wa Afrika Mashariki.

 "Nakumbuka wakati sijaanza muziki nilikuwa nikiona tuzo za Kilimanjaro, natamani zirudi maana zilisaidia wasanii kushindana badala ya kusubiri tu tuzo za nje,” amesema Nandy.

Kuhusu AEAUSA, amesema zimempa heshima kwa kuwa imedhihirika kazi yake inathaminika, “nitazidi kujituma kuona namna gani kazi yake inathaminika na kuongeza zimemuongezea chachu ya kuendelea kujituma zaidi kuliko ilivyo sasa.

Nandy aliwasili uwanjani hapo saa 10 jioni  akiwa amevaa shati jeusi na suruali nyekundu, soksi nyeupe na raba nyekundu na kupokewa na mashabiki zake.

Mashabiki hao walibeba tuzo ya msanii huyo na kupiga naye picha huku wakimsindika katika eneo la kuegesha magari.

Mmoja wa mashabiki hao, Shuga Shugali amesema wamejisikia fahari Nandy kuibuka mshindi huku Marian Hamza akimtaka msanii huyo kuongeza bidii kunyakua tuzo zaidi.