Nassor Mazrui adaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana Zanzibar

Muktasari:

Alikuwa akitokea nyumbani kwake akielekea ofisini. Polisi wamekiri kuwapo kwa tukio hilo.

Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui anadaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana baada ya gari lake kugongwa eneo la Kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi ( JKU).

Inadaiwa baada ya tukio la kugongwa, watu ambao hawafahamiki walimkamata na kutokomea naye kusikojulikana.

Tukio hilo limetokea asubuhi hii ya Jumapili Oktoba 25, eneo la Saateni wakati Mazrui ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ushindi ya kampeni za Maalim Seif Sharif Hamad, akielekea katika ofisi za makao makuu ya ACT-Wazalendo zilizopo Vuga, Unguja.

Katika akaunti ya Twitter ya Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe aliposti taarifa hiyo akitaka watu waliomchukua wamuachie mara moja kiongozi wake anayewania pia uwakilishi katika jimbo la Mwera lililopo mkoa wa Mjini Magharibi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Awadh Juma Haji akizungumza kwa simu na Mwananchi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

"Uchunguzi ukikamilika tutatoa  taarifa zaidi.Kwa sasa siwezi  kulielezea kwa urefu tukio hilo ila ni kweli tumepokea taarifa hizo tumeshaanza kuzifanyia kazi," amesema Kamanda Haji.