Nchi 60 kushiriki maonyesho ya utalii Tanzania

Thursday October 17 2019

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Katibu Mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi anatarajia kufungua maonyesho ya siku tatu ya utalii yanayotarajiwa kuanza kesho Ijumaa Oktoba 18 hadi 20, 2019 katika eneo la Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Maonyesho hayo yaliyopewa jina la Swahili international Tourism Expo (SITE) yatahusisha zaidi ya kampuni za waonyeshaji 210 kutoka nchi 60 na jumla ya wakala wa utalii wa kimataifa 333 wanatarajia kushiriki.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Alhamisi Oktoba 17, 2019 Katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda amesema kwa mara ya kwanza maonyesho hayo yalifanyika mwaka 2014 lakini kila mwaka yamekuwa yakiongezeka ubora na kuchochea ongezeko la watalii kutoka nchi za nje.

“Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za nje wanafanya kazi kubwa sana kututafutia na kuhakikisha tunapata watu sahihi wa kushiriki katika maonyesho hayo na miongoni mwao ni Sweden na Marekani.”

“Nimepita kuangalia maandalizi yanavyokwenda, nimefarijika sana na ninaamini hadi kesho mambo yote yatakuwa tayari,” amesema

Amesema wakati utalii wa dunia ukikua kwa asilimia 6 mwaka 2018 utalii wa Tanzania ulikua kwa asilimia 13 ambayo ni mara mbili ya ukuaji wa kidunia.

Advertisement

“Hii ni kwa sababu Tanzania ni nchi ya amani na imekuwa ikiboresha miundombinu yake ikiwemo barabara, anga na ujenzi wa viwanja vya ndege,” amesema

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii (TTB), Devotha Mdachi amesema baada ya maonyesho hayo mawakala wa utalii kutoka nje ya nchi watapata fursa ya kutembelea vivutio vilivyopo nchini.

“Kuna baadhi wataenda Ngorongoro, Zanzibar, Ruaha, Serengeti ili tu waone vivutio tulivyonavyo na waweze kuvitangaza vilivyo.”


Advertisement