Nchi za EAC zapewa somo kukabiliana na bidhaa kutoka nje

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mhandisi Stephen Mlote akizungumza katika kongamano la biashara lililoandaliwa kwa pamoja kati ya EAC na Bazara la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) jijini Nairobi,Kenya leo.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Iwapo nchi wanachama wa EAC zitapunguza gharama za uzalishaji zitapunguza uingizaji wa bidhaa kutoka mataifa makubwa. EAC inaundwa na Burundi, Kenya, Rwanda, Sudani Kusini, Tanzania na Uganda

Nairobi. Licha ya mafanikio ambayo yamepatikana tangu kuanzishwa kwa Itifaki ya Ushuru wa Forodha, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeaswa kushusha gharama za uzalishaji bidhaa ili kuchochea kupunguza kiwango kikubwa kutokua soko la bidhaa kutoka mataifa makubwa.

Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kanda wa Kenya, Adan Mohamed amesema hayo leo Jumatano Septemba 25, 2019 wakati wa mkutano wa sekta ya biashara ambao ni sehemu ya miaka 20 tangu kuanzishwa EAC.

Amesema kumekua na mafanikio ya kujivunia lakini bado nchi wanachama zinaweza kufanya zaidi ili kuwafanya wananchi wa nchi sita zinaunda EAC kufurahia mtangamano huo.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa EAC, Stephen Mlote amesema yapo mafanikio ya kupigiwa mfano tangu kuanzishwa jumuiya hiyo ambayo yamerahisisha uvukaji mipaka ya nchi wanachama kwaajili ya kufanya kazi, kutoa huduma na kuanzisha biashara katika nchi za EAC.