Nchi za SADC kupiga marufuku usafirishaji wa abiria usio wa lazima

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa nchi 16 za jumuiya hiyo, Profesa Palamagamba Kabudi

Muktasari:

Nchi 16 za mtangamano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),  zimekubaliana kupiga marufuku shughuli za usafirishaji wa abiria usiokuwa wa lazima ndani ya nchi hizo huku zikiruhusu bidhaa muhimu tu kama vile dawa, vifaa tiba, chakula na mafuta ikiwa ni hatua ya kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona(COVID -19) katika nchi za SADC

Dar es Salaam. Nchi 16 za mtangamano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),  zimekubaliana kupiga marufuku shughuli za usafirishaji wa abiria usiokuwa wa lazima ndani ya nchi hizo.
Pili, nchi hizo zimekubaliana kusafirisha bidhaa muhimu tu kama vile dawa, vifaa tiba, chakula na mafuta ikiwa ni hatua ya kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona(COVID -19) katika nchi za SADC.
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa nchi 16 za jumuiya hiyo, Profesa Palamagamba Kabudi ametangaza uamuzi huo leo Aprili 8, 2020 jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kikao cha dharura jana usiku kuhusu mlipuko wa ugonjwa huo.
“Mwongozo huu utawezesha usafirishaji wa bidhaa na huduma muhimu katika nchi za SADC hatua itakayosaidia kuzuia kuenea kwa COVID -19 kupitia usafirishaji mipakani, pia mwongozo utaiizinisha na kuratibu sera, kanuni na hatua za haraka za kitaifa za kukabiliana na corona,”amesema Profesa Kabudi, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
“Naomba kusisitiza wananchi wetu kuzingatia mwongozo huo na miongozo inayotolewa na Shirika la Afya Duniani, mashirika mengine ya kimataifa na wizara ya afya ili kuendelea kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.”
Kikao hicho kilichotanguliwa na kamati ya maofisa waandamizi chini ya mwenyekiti ambaye ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Balozi Kanali, Wilbert Ibuge kiliendeshwa kwa njia ya video.