Nchi za Sadc zajadiliana kuhusu nyuklia

Dar es Salaam.  Mkutano wa kamati ya nishati wa nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) ulioanza leo Februari 25, 2020 nchini Tanzania umeandaa warsha kwa ajili ya kuongeza maarifa kwa watalaam wake.

Mkutano huo ambao ni sehemu ya mwendelezo wa vikao vya Sadc nchini, unahusisha watalaam na makamishina kutoka nchi 12 za jumuiya hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa uamuzi uliopitishwa na mawaziri wanaohusika na masuala ya nishati na wakuu wa nchi.

Itakumbukwa katika mkutano wa 39 wa jumuiya hiyo uliofanyika Agosti 17 na 18, 2019  jijini Dar es Salaam ulikabidhi majukumu ya uongozi wa jumuiya hiyo kwa Rais John Magufuli baada ya Rais wa Namibia, Hage Geingob kumaliza muda wake.

Katika tukio hilo, Tanzania ilianza kuratibu na kusimamia vikao mbalimbali vya kamati za watalaam ikiwamo mkutano huo unaoanza leo.

Kamishna wa masuala ya petroli na gesi wa Wizara ya Nishati nchini Tanzania, Adam Zubery amesema pamoja na warsha hiyo ya Nyuklia, watafanya mapitio, kujadili utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo uanzishaji wa kituo cha umahiri cha kuendeleza nishati jadidifu na matumizi bora ya nishati kwa nchi  za Sadc.

Kwa mujibu wa Itifaki, Kituo hicho kitaanzishwa baada ya kupata angalau uhalali wa wanachama 11 kati ya 16 wa Jumuiya hiyo, kwa sasa kuna nchi nane zilizosaini uanzishwaji wa kituo hicho.

Innocent Luoga, kamishna msaidizi wa umeme nchini Tanzania amesema lengo la uanzishaji wa kituo hicho ni kusaidia kuchochea uendelezaji wa nishati jadidifu katika jumuiya hiyo.

“Watia saini ni 16 lakini wakishafika 11 kituo kinaweza kuanza kazi. Mjadala wa leo kuna taarifa tu itatolewa hadi sasa ni nchi ngapi zimesaini na kuhimizana nchi zilizobaki kusaini,” amesema.