Nchimbi aipeleka Taifa Stars Cameroon

Muktasari:

BAO la straika matata wa Polisi Tanzania, Ditram Nchimbi limetosha kuipeleka timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kucheza Fainali za Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).

Sudan. BAO la straika matata wa Polisi Tanzania, Ditram Nchimbi limetosha kuipeleka timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kucheza Fainali za Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).

Nchimbi, ambaye aliitwa Taifa Stars kwa mara ya kwanza ikiwa ni saa chache tu akitoka kufunga mabao matatu dhidi ya Yanga kwenye sare mabao 3-3 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kuitwa kwake kuliibua gumzo kubwa huku baadhi ya mashabiki wakiamini kwamba, kuifunga Yanga ndio kumempa fursa hiyo, lakini Kocha wa Stars, Ettiene Ndiyaragije alisema ana imani kubwa atakuwa msaada kikosini.

Nchimbi alifunga bao hilo muhimu akimalizia kazi nzuri iliyofanywana Shaban Idi Chilunda aliyekokota mpira na kuingia ndani ya eneo la adui kisha kupiga pasi matata iliyounganishwa vyema na kurejesha shangwe za Watanzania waliokuwa ndani ya dimba la El Merreikh Omdurman na maeneo mengine duniani.

Awali, ilionekana kama Stars ina mlima mrefu wa kupanda kutokana na kumalizika kipindi cha kwanza ikiwa nyuma kwa bao 1-0.

Hata hivyo, kwa sura ya mchezo na kiwango kilichoonyeshwa na Taifa Stars, ilionyesha dhahiri matokeo yanakwenda kupinduliwa kama safu ya ushambuliaji itacheza kwa utulivu.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Taifa Stars wakiendelea kucheza kwa kasi licha ya miundombinu mibovu ya uwanja, kusaka bao la kusawazisha na baada ya ushindi.

Iliwachukua dakika tano tu ya mchezo baada ya kipindi cha pili kwa Taifa Stars kupata bao la kusawazisha kupitia kwa beki kitasa, Erasto Nyoni aliyefunga kwa mpira wa adhabu.

Nyoni alifunga bao hilo kwa ustadi mkubwa akipiga friikiki iliyozama kwenye mwamba wa juu wa goli na kuamuacha kipa akiutazama tu.

 

Bao hilo liliamsha shangwe na kuipa nguvu Stars kusaka bao la ushindi, ambapo benchi la ufundi likiongozwa na Ndiyiragije kusimama mara kwa mara kutoa maelekezo.

Dakika ya 62 ya mchezo Stars ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Iddi Seleman (Nado) na nafasi yake kuchukuliwa na Chilunda huku Miraji Athuman akipumzika kumpisha Ayoub Lyanga ambao, waliipa uhai Stars katika kusukuma mashambulizi.

Pia, Frank Domayo aliyekuwa ameshika dimba la katikati akisaidiana na Jonas Mkude, alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Salum Abubakar katika kusaidia kudhibiti washambuliaji wa Sudan na kupandisha timu mbele.

Kwa upande wao, Sudan ambao kipindi cha kwanza walikuwa wakicheza kwa utulivu huku wakipoteza muda mara kwa mara, walikuwa wakitumia mawinga kusukuma mashambulizi yake huku ikisumbua zaidi upande wa beki Salum Kimenya.

 

Sudan ilipata bao la kuongoza dakika ya 30 ya mchezo wakitumia makosa mabeki wa Stars kushindwa kuwa makini ndani ya eneo lao.

Pia, mabeki wa Sudan hawakuwaruhusu Stars kuingia ndani ya eneo lao la hatari hivyo, kuwafanya Miraji, Nchimbi na Nado kutumia mbinu mbadala kusaka mabao.

Dakika 22 ya mchezo, Stars ilifanya shambulizi la piga nikupige langoni mwa Sudan, lakini jitihada hizo hazikuweza kuzaa bao.

Dakika 24 Domayo aligongeana vyema pasi za haraka na Mzamiru Yassin ambaye aliachia shuti kali lililokwenda juu ya lango.

Kutokana na ngome ya Sudan kuwa ngumu kuingilika, viungo wa Stars waliamua kupiga mashuti makali nje ya 18, lakini Sudan walikuwa makini kulinda lango.

Taifa Stars pia nusura ipate bao la kusawazisha, lakini Miraji alishindwa kuunganisha vyema mpira wa krosi uliopigwa upande wa kulia, ambapo alitakiwa kuunganisha tu kuzamisha wavuni lakini akaupiga vibaya na kurudi uwanjani.

 

Rekodi nyingine kwa Stars

 

Taifa Stars inafuzu kucheza fainali hizi kwa mara ya pili na mara ya mwisho ilikata tiketi yake baada ya kuifunga Sudan kama ilivyofanya jana.

Mwaka 2008, Stars ikicheza na Sudan jijini Khartoum, ilipata ushindi wa mabao 2-1 na kufuzu kwenye fainali zilizofanyika mwaka 2009 ikiwa ni miaka 10 sasa.

Ushindi huo umeongeza rekodi mpya kwa Ndiyiragije, ambaye amevuna ushindi wake wa kwanza ndani ya dakika 90 tangu alipopewa mikoba ya kuwa kocha wa muda.

Pia, Mrundi huyo hajapoteza mechi hata moja akiwa ugenini tangu alipoanza kuinoa Taifa Stars.