Ndege za kivita sherehe za Uhuru zaibua shangwe, hofu

Muktasari:

Licha ya maonyesho ya mwendo kasi na vishindo vya miungurumo mikubwa ya ndege vita za JWTZ kuadhimisha miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika yanayoendelea katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuibua shangwe, nderemo na vifijo kutoka kwa wengi, baadhi ya watu wamekumbwa na hofu hadi kuzimia.

Mwanza. Maonyesho ya ndege vita katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika yameibua shangwe, furaha, nderemo kwa wananchi na viongozi huku baadhi wameingiwa, hofu na woga hadi kuwafanya kupoteza fahamu.

Hali hiyo imetokea leo Jumatatu Desemba 9, 2019 wakati wa maonyesho hayo yanayofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza nchini Tanzania yanakofanyika maadhimisho ya Kitaifa ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika.

Kama mchezo wa kwenye filamu, maonyesho ya ndege vita imeanza kwa ndege tatu kupita kwa kasi juu ya anga na kuibua shangwe kutoka kwa viongozi na wananchi walioko uwanja wa CCM Kirumba unaoingiza watu zaidi ya 25,000.

Kimbembe kikaja baada ya ndege vita zenye miungurumo ya vishindo vilipoanza kukatiza angani na kuzua hofu kwa baadhi ya wahudhuria waliojikuta wakishindwa kuhimili vishindo hivyo na kuzimia kwa hofu.

Wafanyakazi wa huduma ya kwanza kutoka Msalaba Mwekundu wamelazimika kufanya kazi ya ziada kuwabeba na kuwapeleka waliozimia eneo maalum kwa ajili ya huduma.

Baadhi ya waliozimia waliingizwa ndani ya gari la wagonjwa la Jeshi la Wananchi (JWTZ) ambako wamehudumiwa na kuruhusiwa kutoka kurejea kwenye maeneo yao baada ya kurejewa na fahamu.