Ndugai: Wabunge kukaa kwa kutokaribiana si kitu kipya duniani - VIDEO

Muktasari:

  • Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai amewataka wabunge kuzingatia utaratibu wa kukaa mbalimbali (social distance) wakati wote wa vikao vya Bunge kama njia ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona.

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania,  Job Ndugai amesema kuwa utaratibu wa wabunge kuketi bungeni kwa kutokaribiana si kitu kipya katika maisha ya mwanadamu.

 

Akizungumza leo Jumanne Machi 31, 2020 bungeni mjini Dodoma, Ndugai amesema, “wewe ukikutana na mkwe wako huwezi kuegemeana naye, mama akikaa pale na wewe mtu mzima huwezi kwenda kukaa alipo, kukaribiana kunatofautiana baina ya mtu na mtu hata wanyama wa porini wanayo. Mpitie kuku akiwa na vifaranga vyake utaiona shughuli yake.”

 

Amesema wengine wanaona jambo hilo ni shida lakini ni suala linalowezekana na kuwataka kulichukua na kulifuata.

 

Spika amemuagiza katibu wa Bunge kuwapelekea wabunge nyaraka mbalimbali kwa njia ya barua pepe ili popote waliopo waweze kuchangia mijadala inayoendelea.

 

Pia, amewasisitiza wabunge wanaokwenda kwenye mgahawa   kuchukua mahitaji yao na kwenda kutumia mahali pengine bila kumwaga ili kuepusha msongamano katika mgahawa huo.

 

Kuhusu maswali ya nyongeza ya wabunge, Ndugai amesema

fursa hiyo itakuwa kwa wabunge wanaouliza swali la msingi tu na kwamba majibu yatakuwa yamewafikia kabla ya saa 7.00 mchana kila siku.

 

Ndugai amesema wabunge hao watapiga kura katika tablets zao kwa kubonyeza kitufe ambapo yeye atakuwa anaona moja kwa moja mezani kwake kwamba watu wangapi wamekubali bajeti na walioikataa pia.

 

Amesema hata ikihitajika majina atakuwa nayo na kwamba mfumo huo utakuwa wa uhakika na wa moja kwa moja huku akitoa hofu ambayo iliwahi kujengeka kwa baadhi ya watu kuwa utaratibu wa upigaji kura wa awali ulikuwa hauna uhakika.

 

Amesema pia madereva wa wabunge na mawaziri watatengewa eneo nje ya Bunge ili wakishawashusha watoke nje na magari hayo hadi hapo shughuli zitakapomalizika.