Ndugai aitaka Serikali kugawa vifaa vya polisi vilivyokwama bandarini

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai

Muktasari:

Bunge la Tanzania limeagiza makontena ya sare na vifaa vya polisi yaliyokwama bandarini Dar es Salaam yafunguliwe na kugawiwa kwa wahusika haraka.

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameitaka Serikali nchini humo kuanza kuzigawa sare za polisi ambazo makontena yake yamekwama bandarini ili askari waanze kuzitumia.

Ndugai ametoa kauli hiyo wakati akiahirisha mkutano wa 16 Bunge leo Ijumaa Septemba 13, 2019  jijini Dodoma akisema chombo hicho cha kutunga sheria kimejiridhisha nguo hizo ni salama na zinafaa kwa matumizi ya jeshi la polisi

Kauli hiyo ya Ndugai imetolewa ili kuondoa sintofahamu lizokuwepo kuhusu kampuni ya Dalizy iliyopewa zabuni ya kununua nguo hizo za polisi na kuelezwa kulikuwa na sare hewa.

"Katika Bunge lililopita, mlipiga kelele kuhusu makontena yale kwamba yalikuwa hayana kitu, nikateua timu ya wabunge kwa ajili ya kufuatilia jambo hilo na tumejiridhisha mle ndani kuna vifaa vizuri, naagiza wenzetu Serikali muanze kuzigawa haraka sana," amesema Ndugai.

Kampuni ya Dalizy inamilikiwa na Angela Kiziga ambayo kwa muda mrefu ilikuwa na mgogoro kuhusu ununuzi wa sare feki na vifaa vya polisi.