Ndugai akumbushia jinsi alivyomtandika bakora kada wa CCM

Muktasari:

Leo bungeni mjini Dodoma Spika, Job Ndugai amekumbushia jinsi alivyomcharaza bakora kada wa CCM aliyekuwa miongoni mwa wanachama waliojitokeza kuwania kupitishwa na chama hicho tawala kuwania ubunge wa Kongwa pamoja naye


Dodoma. Leo bungeni mjini Dodoma Spika, Job Ndugai amekumbushia jinsi alivyomcharaza bakora kada wa CCM aliyekuwa miongoni wa wanachama waliojitokeza kuwania kupitishwa na chama hicho tawala kuwania ubunge wa Kongwa.

Ametoa kauli hiyo katika kipindi cha maswali na majibu wakati naibu waziri wa elimu, William Ole Nasha akijibu  swali kuhusu viboko shuleni.

Mwaka 2015 katika mchakato wa kura za maoni jimbo la Kongwa, Ndugai alimchapa bakora mwenzake kwa madai kuwa alikuwa akimpiga picha.

"Lakini tukubaliane kuwa bila viboko mambo hayaendi, hata mimi niliwahi kumchapa mtu kiboko," amesema Ndugai na kuwafanya wabunge kuangua kicheko.

Amesema suala la kuchapa fimbo kwa Wagogo na Wamasai ni kitu cha kawaida na watu hawatakiwi kushangaa.

Katika swali la msingi,  mbunge viti maalum (CCM), Zainabu Katimba alihoji kama kuna tafiti zilizofanyika kubaini kuwa adhabu ya kuchapa wanafunzi inaongeza kiwango cha elimu na ufaulu.

Katika majibu yake Ole Nasha amesema tafiti zilizofanyika ndani na nje ya nchi hazijaonyesha moja kwa moja kama viboko vinasaidia au havisaidii.

Hata hivyo amekiri kanuni na waraka wa elimu namba 24 kuhusu adhabu havifuatwi, lakini akasema adhabu kwa wanafunzi zitaendelea kutolewa kwa kufuata utaratibu uliowekwa.