Ndugai asema mbunge anayekataa bajeti ya Serikali ni mpuuzi

Muktasari:

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema mbunge anayekataa bajeti ya Serikali bungeni ni mpuuzi.

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema mbunge anayekataa bajeti ya Serikali bungeni ni mpuuzi.

Ndugai ambaye ni mbunge wa Kongwa (CCM) ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 22, 2019 wakati akiahirisha Bunge la sita la Vijana la mwaka 2019 katika ukumbi wa Pius Msekwa, mjini Dodoma.

Amesema si lazima wabunge wa vyama vya upinzani kuikubali bajeti ya Serikali, kwamba kanuni za chombo hicho cha Dola zinawaruhusu kukaa kimya.

"Kuna mambo matatu katika bajeti, kusema ndio, hapana au kukaa kimya ambako ni ishara ya kuwa hujakataa au  kukubali lakini unasema hapana kwa sauti kubwa hivi unamwelewa mtu huyo kweli," amesema Ndugai.

Spika amesema bajeti zinazokataliwa na wapinzani huwa zimebeba mishahara yao na watumishi wengine,  fedha za miradi ya maendeleo na kwamba kusema hapana ni sawa na kutaka kila kitu kisipelekwe.